NAIBU WAZIRI KUNDO AMTAKA MKANDARASI MRADI WA MAJI MIJI 28 KILWA KUONGEZA KASI YA UKAMILISHAJI WA MRADI

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Methew ametembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 Kilwa Masoko unaojengwa kwa kutumia chanzo cha mto Mavuji unaogharimu dola za Marekeni zaidi ya Milioni 18 sawa na Bilioni 44.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi kutoka Kampuni ya Afcons Infrastructure Ltd na Vijeta Projects and Infrastructure Ltd JV chini ya usimamizi wa mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya M/S WAPCOS Ltd za nchini India.

Akitoa taarifa,Mratibu wa Mradi huo wa maji wa miji 28 kwa upande wa Kilwa Masoko Birune Simon Kawonga kutoka Wizara ya maji ameeleza kwamba,awali mradi ulipangwa kutekelezwa kwa miezi 20 kuanzia Aprili 11,2023 hadi Disemba 10,2024 lakini Mkandarasi ameongezewa muda wa utekelezaji wa miezi 8 kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika usanifu na ujenzi licha ya mpaka sasa kufikia asilimia 68.42 ya utekelezaji.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Omary Nyundo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt.Samia kwa mradi huo ambao unatarajiwa kunufaisha watu zaidi ya 59,983 katika Miji ya Kilwa Masoko na Kilwa Kivinje pamoja na vijiji viwili ambavyo ni Mavuji na Mchakama.

Ujenzi wa mradi wa maji wa Miji 28 kwa Wilaya ya Kilwa utakapokamilika utaongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka wastani wastani wa asilimia 56 kwa miji ya Kilwa Masoko na Kilwa Kivinje hadi kufikia asilimia 96.


 

Related Posts