MATAJIRI wa Azam FC, wamedaiwa wapo katika mchakato wa kuachana na mshambuliaji raia wa Colombia, Franklin Navarro, kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya nyota huyo kushindwa kuonyesha makali yake na kutimiza matarajio yaliyowekwa kwake tangu alipojiunga na timu hiyo.
Navarro mwenye miaka 25, alianza kwa kuondolewa katika usajili wa wachezaji wa kigeni wanaotumika katika ligi kutokana na kukumbwa na majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.
Hata hivyo, baada ya kurejea na kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Azam, kiwango alichonacho hakijamshawishi kocha Rachid Taoussi kumbakisha japo awali aliomba aletewe mshambuliaji mwingine wa kati baada ya Jhonier Blanco kuchemsha na kumtegemea zaidi Nassor Saadun.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani cha Azam, mabosi wa timu hiyo walishafanya vikao kadhaa na kufikia uamuzi wa kuachana na Mcolombia huyo.
“Uamuzi huu haukuwa rahisi, lakini baada ya kumuona Navarro kwa wiki kadhaa, na kutathmini hali ya timu, tuliwaambia mabosi kuwa ingekuwa bora kwa pande zote tukimaliza mkataba huu,” chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti.
Pamoja na hayo, chanzo hicho kiliongeza Blanco naye ana nafasi ya kujitathimini mwenyewe na kuonyesha makali yake katika michezo ijayo ili aepuke uamuzi mgumu kuhusu mustakabali wake.
“Blanco ana nafasi ya kujitetea na kumshawishi kocha na mabosi kuwa anaweza kutoa mchango mkubwa kwa timu katika nusu ya pili ya msimu huu,” kilisema chanzo hicho.
Katika dirisha hili dogo la usajili, Azam FC tayari imetambulisha wachezaji wawili wapya ambao ni beki Zouzou Landry, anayetokea klabu ya AFAD Djekanou ya Ivory Coast, na Zidane Sereri kutoka Dodoma Jiji. Hii ni dalili kuwa Azam wanajipanga kuongeza nguvu katika maeneo muhimu ya timu hiyo ili kuboresha ufanisi wao katika michuano mbalimbali, huku wakijiandaa kushindana na timu nyingine kumalizia msimu.