Nondo za Askofu Bagonza uchaguzi CCM, Chadema

Dar es Salaam. Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vikielekea kufanya mikutano mikuu ya uchaguzi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amebainisha mambo 10 yenye tafakuri tunduizi na hatima ya vyama hivyo.

Januari 18-19, 2025, jijini Dodoma, CCM itafanya mkutano mkuu maalumu utakaoongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan. Pamoja na mambo mengine unakwenda kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti -Bara, iliyoachwa wazi na Abrahaman Kinana.

Nafasi hiyo imekuwa wazi tangu Julai 28, 2024 baada ya Kinana kuandika barua ya kuomba kujiuzulu wadhifa huo kwenda kwa Mwenyekiti wake, Rais Samia, aliyeridhia ombi hilo.

Januari 21, 2025, Chadema katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kitafanya mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi. Freeman Mbowe anatetea nafasi ya uenyekiti aliyoiongoza kwa miaka 21 akichuana na wagombea wengine watatu akiwamo Makamu wake-bara, Tundu Lissu.

Katika uchaguzi huo wenye mchuano mkali, wajumbe wa kamati kuu, John Heche anawania umakamu mwenyekiti-bara akimuunga mkono Lissu. Ezekiel Wenje ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Viktoria anawania umakamu mwenyekiti-bara akimuunga mkono Mbowe.

Mikutano hiyo yote ya vyama vinara nchini inafanyika Januari hii, ikiwa ni maandalizi ya vyama kuweka safu za uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani inaotarajia kufanyika Oktoba 2025.

Kutokana na mikutano hiyo, Askofu Bagonza amechambua mambo 10,  katika andiko lake aliloliweka kwenye kurasa zake za kijamii kiongozi huyo wa kiroho anatafakarisha kinachoendelea Chadema ama akiita kwa kifupi ‘CDM’ na CCM. Andiko lake amelipa kichwa cha habari ‘Januari 2025: CCM, CDM kumbukeni kuna nchi.’

Askofu Bagonza ameandika…

Vyama vikubwa viwili hapa nchini, CCM na CDM vina mikutano mikuu mwezi huu wa Januari 2025. Wakati CDM inakamilisha chaguzi zake za ndani ngazi ya kitaifa, CCM itamchagua Makamu Mwenyekiti (Bara) kufuatia kujiuzulu kwa kada mwaminifu wa muda mrefu wa CCM Komredi Abdulrahaman Kinana.

Yako mambo kadhaa inabidi yaongoze fikra za wanachama wa vyama hivyo lakini pia Watanzania kwa ujumla kwa sababu, vyama hivi vimeshikilia sarafu ya shilingi ya Watanzania kwenye tundu la choo.

CDM ina mashabiki wengi kuliko wanachama. Itafanya kosa kubwa kufikiri mawazo ya viongozi ndiyo ya wanachama na mashabiki.

Pia, CCM ina wanachama wengi kuliko mashabiki. Itafanya makosa makubwa kufikiri mawazo ya wanachama wake ndiyo mawazo ya nchi.

Vilevile, mbele ya CCM, CDM kinaonekana kama shetani aliyebeba habari njema. Ndiyo maana kada wa CDM akihamia CCM anapewa uongozi bila semina elekezi.

Mbele ya CDM, CCM kinaonekana kama malaika aliyebeba habari mbaya. CDM wanaona CCM ina fursa zisizotumika kubadili maisha ya watu. Ndiyo maana CDM inakazana na agenda mpya (katiba mpya, uhuru wa tume za uchaguzi).

Askofu Bagonza anaendelea kueleza kuwa, agenda ya mabadiliko katika chaguzi na mikutano ya CDM na CCM mwezi huu wa Januari 2025, inavichanganya vyama vyote. Mabadiliko ni tishio na ni fursa.

Anaeleza,  mashabiki na wanachama wa CDM wanaelekea kuchagua mabadiliko hata kama yatakiua chama kwa tumaini la ufufuko. Masikio yasiyosikia sauti hizi hayahitaji dawa. Tumaini la ufufuko ni gumu lakini ni msingi wa dini fulani inayoheshimiwa hata na wanaoipinga.

Katika andiko hilo aliloliweka kwenye mitandao ya kijamii, Bagonza anaendelea kufafanua kuwa,  viongozi wengi wa CDM wanaelekea kutafakari tishio la mabadiliko kuliko fursa ya mabadiliko. Wanasema “Shetani uliyemzoea ni bora kuliko malaika wa ahadi.” Tishio la kumpoteza ‘shetani’ na wasimpate ‘malaika’ linawatafuna.

Anaeleza, CCM inauwazia uchaguzi wa CDM kuliko uchaguzi wa Makamu wake. Watanzania huichagulia CCM Mwenyekiti na kisha Mwenyekiti huyo huichagulia CCM Makamu wake. Wajumbe wanaenda Dodoma kukagua maendeleo ya jiji la Dodoma. Kimsingi, Makamu Mwenyekiti wa CCM ndiye Mwenyekiti ‘kivuli’ CCM ili kumpa ‘Mwenyekiti-Rais’ nafasi ya kuongoza nchi. Kwa hiyo CCM na CDM wanachagua wenyeviti mwezi huu.

Bagonza anaeleza, wagombea wa CDM wamekaa kwa ‘uzembe wa kimkakati’. Hii timu Lisu/Heche dhidi ya timu Mbowe/Wenje ni kama mtego wa panya. Matokeo yakiwa Lisu/Wenje au Mbowe/Heche, demokrasia itaingia majaribuni. Bahati mbaya, ni rahisi kuingia mbinguni kuliko kusajili chama kipya Tanzania.

“Ukweli mchungu: CCM inaihitaji CDM imara kuliko inavyolihitaji kundi moja ndani ya CDM. CDM dhaifu ni sumu ya CCM. Na CDM inayahitaji mawazo ya mashabiki kuliko ya viongozi. Taifa imara linaihitaji CCM na CDM imara. CCM acheni kiburi na CDM acheni utoto,”anaeleza Askofu Bagonza kwenye andiko hilo.

Anaeleza, palipoandikwa CDM unaweza kuweka ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi n.k na maana itabaki ileile. “Palipoandikwa CCM ondoa Polisi mawazoni mwako ibaki CCM peke yake,”.

Related Posts