ONGEA NA ANTI BETTY: Mke wangu ananificha mimba yetu

Swali: Kuna vitu Antie nashindwa hata kuamini, inawezekanaje mkeo akufiche kuhusu kuwa na mimba ambayo bila shaka wewe ni mhusika! Nashangaa mke wangu ananificha mimba yetu, inawezekanaje.

Huu ni mwezi wa tatu ninaona mabadiliko ya kitabia kwa mke wangu, kiasi nikahisi ana mimba, nikatenga muda tumetulia nikamuuliza mwenzangu kwema? Akanijibu kwa ukali kidogo kwema, kwani vipi? Nikamwambia moja kwa moja nakuona kama una mimba. Akakataa. Zikapita siku tatu akawa anapata joto la mwili (homa) kila ikifika jioni, nikimwambia nimpeleke hospitali hataki.

Juzi nikawa nina kikao ofisini cha mapema hivyo nikamwambia kuwa kesho amwambie ndugu yake ajipange maana sitotoka naye kwani nitatoka mapema sana kwenda kazini kuwahi hicho kikao. (ndugu yake huwa nampa lifti hadi kazini kwake kwa sababu njia yetu ni moja).

Hapohapo mke wangu akasema ataongozana na mimi nikamuache hospitali akapate vipimo kwani anajisikia vibaya na jioni anapata homa, nikashangaa kwani kila nikimwambia nimpeleke hataki. Nikatoka naye siku iliyofuata nikamuacha hospitali nikawahi kikao, jioni nilipomuuliza ameambiwaje, akasema kaambiwa ni uchovu tu, anywe maji mengi na apumzike. Sikumuuliza zaidi nikamuacha ila sikuwa nimeridhika na majibu yake, kwani kila nikimtazama namuona kabisa ana mimba.

Sasa nimejuaje kama anayo kweli, unaweza kushangaa hata wewe, Mungu yupo upande wangu katika hili. Nilikuwa najiweka vizuri kola ya shati kwenye ‘dressing table’ pembeni kuna kidude kidogo cha kuweka takataka, nikaona karatasi la hospitali lile ambalo ukilipa bima unapewa, nikavutiwa nalo nikalichukua, lilikuwa limechanwa vipande vipande, ila nilichokipata kilikuwa na baadhi ya majibu ya vipimo ikiwamo hicho cha ujauzito, nikaunganisha makaratasi mengine nikapata jina la mke wangu, nikajua ni majibu yake.

Huwezi kuamini nilipomuuliza kesho yake kuhusu kama ana mimba au la alikataa na ndiyo kwanza anataka kwenda kwao kusalimia.

Sijui hata ana nini, pia anajitenga na mimi tangu nirudi safari kama miezi miwili iliyopita, nikahisi ananiogopa anadhani nina maradhi kwa sababu nilikaa huko safarini miezi mitatu.

Naomba ushauri, kwani nashangaa sana mke kumficha mimba mumewe, kuna wakati ninapata mawazo mabaya ila nayapotezea kwa sababu nampenda sana mke wangu.

Jibu: Duh! Hili siyo swali ni simulizi. Ila hakijaharibika kitu, natamani ungesema unawaza mambo mabaya yapi? Kwa kuwa hujayataja tuachane nayo. Ila binafsi nina mashaka na mkeo kuhusu hiyo mimba, hakuna mwanamke anayemficha mimba mumewe.

Lakini pia kuna wanawake kutokana na mabadiliko ya mwili baada ya kupata mimba wanakuwa wakorofi, wakali, wanawachukia watu bila sababu na wengine huwachukia waume zao.

Pengine na mkeo amepata hiyo changamoto ndiyo maana anakuficha, kwa maana hayupo sawa hafikirii kama ilivyokuwa zamani. Kwanza ongeza ukaribu naye ili ujue ukweli wa hiyo hali, kama ulikuwa ukirudi kazini unapita mahali kubadilishana mawazo na washikaji sasa rudi nyumbani moja kwa moja.

Pia fuatilia nyendo zake, inawezekana ana mawazo mabaya kuhusu hiyo mimba ndiyo maana anakuficha. Ukitulia kaa naye chini mueleze ulichobaini kupitia karatasi za vipimo ulizoziona ndani.

Mazungumzo yaanzie hapo, anaweza kukubali au kukataa, akikubali muulize kwa nini alikuwa anakuficha anaweza kukupa sababu. Akikataa hapo ndiyo ushirikishe jamaa zake, wakiwamo ndugu wa karibu ili akapimwe kama anayo kweli na majibu yakiwa anayo aeleze kwa nini anakanusha.

Majibu yakionyesha hana, utatoa ushahidi wa vipimo ulivyoviona amevichana vikiwa na jina lake.

Kisha yeye ndiyo atamaliza huo utata kwa kueleza ana maana gani kufanya yote hayo, mwenye majibu ya hili ya moja kwa moja ni mkeo, wewe muandalie mazingira ya kukujibu kama nilivyokuelewesha hapo juu.

Ukiwa na moyo wa subira vumilia tu, kwani mimba ni pembe la ng’ombe haifichiki itaonekana tu

Related Posts