NA WAF
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutekeleza mkakati wake wa kuimarisha huduma za dharura nje ya hospitali kwa kushirikiana na wadau binafsi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu alipotembelea moja ya wadau wa Sekta binafsi wanaotoa huduma za Dharura kampuni ya Emergency Medical Services inayofahamika kama E-Plus Tanzania, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam ambayo ni miongoni mwa kampuni zinazotoa kutoa huduma za Dharura kupitia Ambulance nchini.
Dkt. Jingu amesema kuwa, E-Plus imekuwa ikishirikiana na Serikali kuhakikisha huduma za dharura zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaotakikana.
“Nimewasikiliza na kupokea maoni yao juu ya baadhi ya maeneo ambayo wanategemea Serikali iwasaidie ili waweze kufanya kazi vizuri na sisi kwa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba tunawezesha Sekta binafsi na yenyewe kutoa mchango wake katika maeneo yote ambayo wanapaswa kufanya au wamejikita kufanya kazi hiyo. Basi na sisi tunatekeleza majumu yetu kuhakikisha wanafanya vizuri katika upande huu wa huduma za afya za kidharura.” Amesema Dkt. Jingu.
Katika ziara hiyo, Dkt. Jingu ameweza kujionea huduma mbalimbali ikiwemo chumba maalum cha kupokea taarifa za dharura na zisizo za dharura kwa saa 24 (Dispatch room), chumba cha Vifaa vya huduma ya dharura na kushuhudia Ambulance yenye Vifaa ambayo ni kama ‘ICU inayotembea’.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba wa E-Plus Tanzania, Dkt. George Pondo amesema
wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ili kufikia malengo makuu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuokoa Maisha ya Watanzania, hususan wakati wa dharura za kiafya.
“Tuna magari ya dharura ya kisasa yenye huduma bora na vifaa vyote na tupo tayari kushirikiana na Serikali na wenzetu katika Sekta binafsi kutoa huduma kwa Watanzania wote kwa kuwa kila mtu anayo haki ya kupata huduma ya ambulance kokote ndani ya Tanzania. Maisha ni muda”. Amesema Dk. Pondo.
Hii ni sehemu ya ziara inayoendelea ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya kukagua utekelezaji wa mkakati wake wa kuimarisha huduma za dharura nchini zikiwemo dharura nje ya hospitali kupitia magari ya wagonjwa (ambulance) na mifumo ya kidijitali ya uratibu wa magari ya wagonjwa inayoendelea kuimarishwa nchini.