Serikali yaanza kuwapokea vijana 420 wa BBT awamu ya pili

Dodoma. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kuwapokea vijana wa awamu ya pili wa mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ambapo wanatarajia kupokea vijana 420 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Januari 12, 2024 Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Bajeti wa Wizara wa Kilimo, Mohamed Chikawe amesema awamu hii wanatarajia kuzalisha tani zaidi 8400 za mbegu bora ya mahindi aina ya C105 katika  ekari 4,200 walizoziandaa.

Chikawe amesema awamu hii wameandaa eneo la Ndogoye lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwapeleka wanufaika hao.

Amesema kila kijana mmoja atakabidhiwa ekari 10 kwa ajili ya uzalishaji wa aina hiyo ya mbegu itakayotumika katika msimu ujao wa kilimo.

“Mpaka sasa tumeshapokea vijana 209 na bado wanaendelea kuwasili,”amesema Chikawe.

Amesema vijana hao wanakwenda kuzalisha mbegu za mahindi aina hiyo ya C105 ambazo zitakuwa mbegu bora kwa sababu watazalisha chini ya usimamizi wa wataalamu wa kilimo kutoka taasisi za uzalishaji mbegu bora.

Hata hivyo, amesema maandalizi kwa ajili ya kuwapokea vijana hao yamekamilika na kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya kilimo kipo kilichobaki ni kuanza uzalishaji.

Kwa upande wake mmoja wa vijana hao, Ilumbo Yohana kutoka wilayani Chamwino amesema wanakwenda kutumia fursa hiyo ya kilimo kama zawadi kwao, ili kuwainua kiuchumi wao wenyewe na kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya kilimo.

“Kilimo ni fursa kubwa kwa vijana hasa ukizingatia Serikali imewekeza kwenye sekta hiyo hivyo vijana tunapaswa kuchangamkia fursa kama hizi zinazotolewa na Serikali,” amesema Ilumbo.

Naye Fanuel Buu kutoka wilaya ya Babati mkoani Manyara amesema anashukuru jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia sekta ya kilimo.

Related Posts