Zanzibar inapoadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi yake, Taasisi ya Ofisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (ZPDB), inajivunia kuchangia mafaniko makubwa katika maendeleo ya Taifa, ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake.
Taasisi hii iliyopo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu, ilianzishwa na kuzinduliwa rasmi Desemba 2, 2022 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Taasisi ya ZPDB ina lengo la kuifuatilia, kuisimamia na kuisaidia Serikali katika utendaji na utekelezaji wa miradi ya kipaumbele.
Wakati akiunda taasisi hiyo, Rais Mwinyi alisema kupata mafanikio kunahitaji vipaumbele na shabaha zinazoweza kupimika, pia kuwepo mipango makini na ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kutatua matatizo yanayojitokeza kuondoa ucheleweshaji wa kazi na maendeleo.
Katika muundo wa ZPDB, viliwekwa vipaumbele katika maeneo manne aliyotaka kuanza nayo kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji na usimamizi wa ahadi zake kwa wananchi wa Zanzibar.
Maeneo hayo ni miundombinu, utalii, uchumi wa buluu (uvuvi na ukulima wa baharini, mafuta na gesi, shughuli maalumu za utalii, usafiri na usafirishaji baharini).
Maeneo mengine ni huduma za kijamii (afya, elimu, majisafi na salama na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi).
Katika muundo wa ZPDB, pia kuna sekta wezeshi ambazo ni mawasiliano na habari, fedha na utafutaji rasilimali, Tehama na sheria.
Mtendaji Mkuu wa ZPDB, Profesa Mohammed Hafidh Khalfan anasema katika kipindi cha miaka miwili ya utendaji wa taasisi hiyo, yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Imani ya wananchi imeimarika kwa kuona vipi Rais wao anawajali kwa kuunda Taasisi maalumu kushughulikia mahitaji yao na maendeleo endelevu ya nchi.
ZPDB haifanyi kazi peke yake, inashirikiana na Wizara na Taasisi mbalimbali za SMZ na Taasisi nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kama vile Sema na Rais (SNR), Taasisi ya Nyaraka na ile ya Serikali Mtandao (eGAZ).
Moja ya mafanikio ni kuelimisha umma kuhusu nini Rais amefanikisha katika kipindi cha muda mfupi wa uongozi wake (miaka minne kama mia nne).
Mafanikio ni mengi, lakini miongoni mwa mafanikio maalumu yaliyosajiliwa na ZPDB tangu kuanzishwa kwake kupitia sekta mbalimbali ni pamoja na kusimamia utekelezaji katika sekta zifuatazo:
Uchumi wa Buluu; kuimarika kwa huduma za usafiri na usafirishaji wa baharini ndani ya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba, zikiwemo bandari zetu na miji ya jirani.
“Na kwa sifa maalumu, tunamshukuru Rais, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kufanikisha Bandari ya Mkoani kupokea meli za makontena moja kwa moja kutoka nje ya nchi.
“Hii itaimarisha biashara za ndani na nje ya nchi, sambamba na kuwekeza katika kiwanda cha mwani ambacho kitaanza kazi ndani ya mwaka 2025.”
Kiwanda hiki kitasaidia kuwa na soko la uhakika kwa wakulima wa mwani na kuongeza thamani ya zao hili kuanzia ununuzi kutoka kwa wananchi hadi kuusarifu na kuuza bidhaa zake nje ya nchi; Kujenga viwanda vya kusarifu dagaa katika eneo la Kama (Unguja) na Ndagoni (Pemba).
Miongoni mwa mafanikio ya huduma za jamii ni ujenzi wa miundombinu ya elimu, ikiwemo madarasa mapya na skuli mpya, zikiwemo za ghorofa. Sasa zaidi ya madarasa 1,500 yameshajengwa.
Ujenzi wa miundombinu ya afya, ikiwemo hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa, nyumba za madaktari kisiwani Pemba, kuipa sekta binafsi ushiriki wa utoaji wa baadhi ya huduma na hivyo kuimarisha huduma wanazopata wananchi.
Mengine ni uanzishwaji wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar, uwekaji na uimarishaji wa miundombinu ya maji Unguja na Pemba na upatikanaji wa takwimu za ajira kupitia wizara husika na ZEEA.
“Tumeshuhudia kuendelea kuimarika miundombinu nchini, ikiwamo ya bandarini, viwanja vya ndege, barabara, mawasiliano.”
Anasema miundombinu imeimarika zaidi kupitia kusainiwa kwa mkataba wa usimamizi wa bandari ya Malindi kwa wawekezaji AGL/ZMT.
Kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa bandari ya Fumba, ukarabati wa Bandari ya Mkoani – Pemba, ujenzi wa Bandari ya Shumba – Pemba na maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Wete – Pemba nayo ni mafanikio.
Mafanikio mengine katika miundombinu ni ujenzi wa majengo ya biashara, Terminal II na VIP katika eneo la uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Unguja na mchakato wa maandalizi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Pemba, bila kusahau ujenzi wa barabara mbalimbali za Unguja na Pemba (mijini na vijijini).
Miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa watalii hadi kufikia 736,000 mwishoni mwa Desemba 2024, huku jitihada zikiendelea katika uanzishwaji wa soko jipya la Halal Tourism kwa Zanzibar.
Profesa Khalfan anasema yamefanyiwa ukarabati na uimarishaji maeneo ya kihistoria na ya urithi, kusainiwa mkataba wa Touch Road na China ili kupata soko kubwa la kutoka China na upatikanaji wa haki za mwekezaji wa Kisiwa cha Bawe ambapo sasa uwekezaji mkubwa unafanyika.
Mafanikio mengine ni ukarabati wa Ngome Kongwe na bustani za Africa House, kubadilisha Mahakama Kuu ya Vuga kuwa Makumbusho ya Mahakama ya Zanzibar na kuanzisha mashindano ya “kitesurfing” Zanzibar pamoja na ukarabari wa makumbusho ya Amani.
ZPDB imeanzishwa kwa lengo maalumu, haitarajiwi kuwa taasisi ya kudumu.
“Tuna imani katika kipindi kisichozidi miaka mitano, ile dhamira ya kuanzisha ZPDB itakuwa imefikiwa na utendaji katika taasisi za Serikali ambazo zitaweza kujisimamia zenyewe kuanzia ngazi za chini hadi za juu za kiwizara,” anasema
Anasema malengo muhimu na vipaumbele vya Serikali havitekelezwi kwa haraka na kwa kiwango kinachohitajika ili kukidhi mahitaji ya wananchi na nchi kupiga hatua stahiki za maendeleo endelevu na ndiyo sababu ya kuanzishwa taasisi hiyo.
Ni muhimu kuelewa, ZPDB si taasisi tendaji zinazoshughulika na miradi ya vipaumbele.
Profesa Khalfan anasema ZPDB inasimamia utendaji na inasaidia katika kutafuta rasilimali ili kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo kwa mujibu wa malengo makuu ya nchi.