Rais mteule wa Marekani, Donald Trump leo Jumapili Januari 12, 2025 amewakosoa vikali maafisa wanaosimamia juhudi za kuzima moto mkubwa unaoendelea kuteketeza Los Angeles, akiwaita ‘watu wasio na uwezo’ na kuhoji kwa nini moto huo bado haujazimwa.
“Moto bado unaiteketeza L.A,” aliandika Trump kwenye mtandao wake wa Truth Social.
“Wanasiasa hawa wasio na uwezo hawajui hata namna ya kuuzima.”
Kauli hizi za Trump zinaonyesha kuwa masuala ya moto huu na jinsi maafisa wanavyokabiliana nao huenda yakawa sehemu muhimu ya ajenda yake ya kisiasa ya ndani atakapochukua madaraka rasmi mnamo Januari 20.
Pia, ameendeleza ugomvi wake wa muda mrefu na Gavana wa California, Gavin Newsom, ambaye naye amemshutumu Trump kwa kuligeuza janga hili kuwa suala la kisiasa.