Ndoa ni muungano mtakatifu unaopaswa kuwa huru na usiotegemea au kuingiliwa na watu wengine.
Wakati wa kuapishwa, waliokula kiapo ni wawili tu na si miambili. Hivyo, jukumu la kutunza kiapo chenu ni lenu wenyewe.
Si jukumu la watoto wenu, wazazi, marafiki, mashoga, au wengine, hata kama mnawapenda, kuwathamini, au kuwaamini vipi.
Ndoa ni kama sehemu zenu za siri; hazipaswi kufahamika na mtu mwingine isipokuwa ninyi wenyewe. Mnalo jukumu la kuilinda, kuitunza, na kuiimarisha ndoa yenu.
Ikiwa mtaiachia ivunjike, sababu itakuwa ni kushindwa kwenu kutimiza wajibu wenu. Hakuna anayeweza kuzihudumia sehemu zenu za siri au kuziona isipokuwa ninyi wawili. Je, nani mpumbavu huanika chupi zake hadharani?
Hii inasisitiza kuwa ndoa inapaswa kuwa taasisi huru, yenye uhuru wa kweli wa kutoingiliwa na yeyote.
Uamuzi wa jambo lolote linalowahusu wanandoa linapaswa kuwa la wanandoa wenyewe pekee na halipaswi kuwa shinikizo au ushawishi wa nje.
Mfano wa Athari za Kutoa Siri
Mwanandoa mmoja mzembe alizoea kusimulia siri za mwenzi wake kwa marafiki zake, ikiwamo maelezo ya maumbile yake na ujuzi wake wa kimapenzi.
Miongoni mwa hao marafiki walikuwemo watu wakware waliokuwa wakimmezea mate mwenzi wake.
Siri hizo ziliposambaa, zikawa chanzo cha anguko la ndoa yake, kwa sababu njama zilitengenezwa dhidi ya mwenzi wake na hatimaye ndoa hiyo ikavunjika na watesi wakashangilia.
Kwa maana nyingine, hili ni somo kubwa kwa wanandoa kwamba, binadamu hupenda zaidi maslahi yake binafsi, hata kama yanawaumiza wengine.
Na hapa kuna somo kubwa kwamba mafanikio ya ndoa yako ni siri yako; si kitu cha kusimulia kwa wengine. Kama ilivyo kwenye methali isemayo, “Siri ya mtungi aijuaye kata,” ndivyo inavyopaswa kuwa kwa ndoa yako pia.
Linapotokea tatizo ndani ya ndoa, ni muhimu lifanyiwe kazi na wanandoa wenyewe, tena kwa usiri mkubwa.
Lakini pia ni vizuri wanandoa hawa wakatambua kwamba siri za chumbani zisivushwe hadi sebuleni.
Na kama hali itazidi, ni vizuri wawili hao wakawashirikisha wazazi wa pande zote mbili, lakini kwa umakini na ikiwezekana wawashirikishe pia viongozi wa dini badala ya kuanika matatizo yenu kama mnatangaza biashara fulani.
Wazazi wanaweza kutoa ushauri kutokana na uzoefu wao, lakini bado thamani na umuhimu wa ndoa yenu unajulikana zaidi na ninyi wenyewe.
Hata hivyo, tahadhari lazima ichukuliwe. Si kila mzazi anaweza kuwa na uwezo wa kushughulikia matatizo ya ndoa kwa ufanisi, hasa ikiwa walikulia kwenye ndoa za mitala au zilizojaa matatizo.
Ndoa ni jukumu lenu wawili. Kushirikisha watu wa nje mara kwa mara huchangia kuongeza changamoto badala ya kuzitatua.
Mlipoamua kufunga ndoa, mlikuwa peke yenu na wengine walikuwa mashahidi tu.
Wakati wa matatizo, msikimbilie kwa wapambe au mashahidi wenu kwa sababu mara nyingi hawana nia njema, uzoefu, au ufahamu wa kutosha kuhusu mahusiano yenu.
Msimamo wa ndoa unatokana na wanandoa wenyewe. Changamoto na matatizo ya ndoa yachukuliwe kama sehemu ya safari yenu.
Hakimu wa kwanza wa matatizo ya ndoa ni wanandoa wenyewe, na mahakama yao ni chumba cha kulala. Linda, tunza, na imarisha ndoa yako kwa hekima, usiri, na uwajibikaji.