UWAVITA WATAKA DIRA YA 2050 KUENDELEZA TASNIA YA VITABU

Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA),  Anna Mbise, amesema umoja huo umeshiriki kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025-2050 ikiwa ni mwitikio wa wito wa Serikali unaoshirikisha taasisi na wananchi katika mchakato wa kupata maono ya pamoja kwa maendeleo ya nchi miaka 25 ijayo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Uwavita imepokea maoni kutoka kwa wanachama wake nchi nzima na kwamba maoni hayo yamebeba mtazamo wa kuendeleza tasnia ya uandishi wa vitabu nchini kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hiyo katika kuchochea maendeleo endelevu.

“Maoni ya wanachama wa UWAVITA tayari yamewasilishwa kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kwa ajili ya hatua zinazofuata. Umoja umejikita katika kuhakikisha kuwa maoni yake yanatoa mchango wa kina kwa ukuaji wa tasnia ya vitabu na fasihi kwa ujumla nchini,” imesema taarifa ya Uwavita kwa wanahabari.

Taarifa imesema kwamba Katiba ya Uwavita, Ibara ya 12 kifungu (L), inasisitiza jukumu la umoja huo la kushauri serikali juu ya sera bora zinazohusiana na sekta ya vitabu na fasihi.

Bi Anna katika taarifa hiyo amesisitiza kuwa UWAVITA ni taasisi imara iliyo na dhamira ya kuwajengea uwezo waandishi wa vitabu nchini ili kuhakikisha wanatoa kazi bora zinazosaidia maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

 

Related Posts