Wastani pato la Mtanzania wafikia Sh3.05 milioni kwa mwaka

Dar es Salaam. Pato la mtu mmojammoja nchini limeongezeka hadi kufikia wastani wa Sh3.055 milioni kwa mwaka 2023, Ripoti ya mwaka 2023/2024 iliyotolewa na Benki kuu ya Tanzania (BoT), inaeleza.

Ongezeko hili ni ukuaji wa miaka saba mfululizo ikitoka Sh2.32 milioni mwaka 2017 hadi kufikia ilipo sasa.

Ukuaji huu wa wastani wa pato la mtu mmojammoja unaenda sambamba na ukuaji wa pato la Taifa  (GDP) ambalo lilifikia Sh188.58 trilioni mwaka 2023 kwa thamani halisi ya sasa kutoka Sh118.74 trilioni, mtawaliwa.

Uchambuzi unaonyesha kuwa, shughuli za kiuchumi kwa ujumla zilichangia Sh175.78 trilioni katika pato la Taifa kiwango ambacho kiliongezeka kutoka Sh108.95 trilioni mwaka 2017.

Kiasi kilichobakia cha Sh12.8 trilioni kilitokana na kodi iliyotozwa katika bidhaa mbalimbali.

Ukuaji wa GDP kwa mtu mmojammoja upande wa Tanzania Bara ni wa chini kidogo ikilinganishwa na Sh3.11 milioni kwa wakazi wa Zanzibar ambayo pia ni ukuaji kutoka Sh2.3 milioni waliyokuwa nayo mwaka 2018.

Uchangiaji wa shughuli mbalimbali katika GDP

Taarifa hii iliyochapishwa Desemba 11 mwaka jana inaeleza kuwa, huduma mbalimbali zilizotolewa nchini zilichangia Sh69.81 trilioni huku ikiongozwa na biashara za jumla na rejareja iliyochangia Sh15.6 trilioni, huku sekta usafiri na uhifadhi ikichangia  Sh13.5 trilioni.

Sekta ya ujenzi na biashara ilichangia Sh55.9 trilioni huku shughuli za ujenzi pekee zikichangia Sh24.9 trilioni.

Kundi lingine lililochangia katika GDP ya Taifa ni kilimo, uwindani na misitu ambayo ilikuwa na Sh49.97 trilioni huku mazao yakiwa na zaidi ya Sh30.37 trilioni.

Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa biashara na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai amesema uchumi unavyokua pato la mtu linaweza kuongezeka, lakini inategemea na sekta ambazo zimechochea ukuaji huo kwa namna gani zinamgusa Mtanzania moja kwa moja.

“Pato linaweza kukua lakini hali ya umasikini ikakua au ikabaki palepale. Ila pato linapoongezeka katika uchumi ni ishara nzuri ambayo itawafanya watu kufikiria kuwekeza kwa sababu ya uwezo wanaokuwa nao, hii inaenda sambamba na kukua kwa uwezo wa watu wa kununua bidhaa na huduma mbalimbali,” amesema Dk Swai.

Amesema ukuaji wa wastani wa pato la Mtanzania pia inasaidia watu kuwekeza katika mifumo mbalimbali ikiwemo ule wa Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) au kuwasukuma kutumia huduma za kifedha kwa kufungua akaunti za benki.

“Kuna viashiria ambavyo vinaonyesha kuwa pato la mtu limekuwa miongoni mwake ni maendeleo ya teknolojia ambayo yamewezesha ubunifu ambao unaweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa miundombinu pia unafanya watu kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na kufikia masoko,” amesema Dk Swai

Katika hilo, Dk Swai alitoa rai kwa taasisi za fedha kuweka nguvu katika kuhudumia watu wa vijijini zaidi na kuwekeza katika uvumbuzi unaofanyika,  ili uweze kusaidia kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Haji Semboja amesema ukuaji wa wastani wa pato la mtu kwa Mtanzania inamaanisha kuwa idadi ya watu wanaojishughulisha katika kutengeneza kipato imeongeza, hali ambayo ametaja kuwa inaonekana katika miji ikiwamo Dar es Salaam kwa namna wanavyojishughulisha.

“Siku hizi katika barabara mbalimbali na hata majumbani watu wamekuwa wakipita kuuza bidhaa tofauti na zamani,” amesema Profesa Semboja.

Hata hivyo, wananchi wenyewe wanashangaa kukua kwa wastani wa pato lao kwa mwaka, huku wakisema hali za maisha kwa mtu mmojammoja bado ni duni.

“Ukisema pato la mtu limekuwa maana yake anaweza kumudu gharama za maisha lakini kuna watu bado wanakula kwa taabu tena mlo mmoja, huyu tunamuweka kundi gani, tusitumie ukuaji wa uchumi wa watu wengine kuwajumuisha wote,” amesema Lianga Msemo mkazi wa Tabata.

Maneno yake yaliungwa mkono na Venance Urio ambaye amesema ni vyema sekta zinazoajiri watu wengi zikaboreshwa zaidi ili kuongeza uwezo wa watu kumudu mahitaji ya msingi kwa familia zao.

Ametolea mfano wa kilimo ambacho kinaajiri watu wengi, bado tija yake ipo kwa kiwango kidogo hivyo ni vyema uimarishaji zaidi ukafanyika.

“Kufanya hivi tutaondoa uchumi wa kwenye makaratasi na kuuleta katika mifuko ya watu, huu ndiyo wakati ambao ukizungumza uchumi kukua watu hawatakua na kelele kwa kudhani kuwa unadanganya,” amesema Urio.

Wakati hayo yakisemwa, Januari 8, mwaka huu, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alisema mwaka 2025 ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara na Zanzibar unatarajiwa kukua kwa takribani asilimia 6 na asilimia 6.8 mtawalia.

Ukuaji huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na

ugavi, nishati ya uhakika pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.

Hii linatabiriwa wakati ambao mwaka 2024, uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya nne ya mwaka 2024.

“Kwa kuzingatia mwenendo huo, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwa sawia na maoteo ya ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2024. Ukuaji huu umechangiwa zaidi na ongezeko la shughuli za kilimo, usafirishaji, ujenzi na biashara,” alisema Tutuba.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8 katika robo ya kwanza na asilimia 7.2 katika robo ya pili ya mwaka 2024 na unakadiriwa kukua kwa viwango hivyo kwa robo mbili zinazofuata, hivyo kufikia maoteo ya ukuaji wa asilimia 7.2 kwa mwaka 2024. Shughuli zilizochangia zaidi ukuaji huu ni utalii, ujenzi na viwanda.

Related Posts