BAADA ya kushusha majembe matatu kwenye dirisha dogo la usajili, Yanga Princess imesema bado wengine wanakuja.
Hadi sasa Yanga imetambulisha wachezaji watatu kutoka Get Program, Diana Mnally, Zubeda Mgunda na Protasia Mbunda ambao hapo awali Mwanaspoti tuliwahi kuandika kuhusu tetesi za wachezaji hao kuhusishwa na wananchi wa kike.
Msimu huu Yanga Princess chini ya Edna Lema ‘Mourinho’ imecheza mechi nane, ushindi tatu, sare tatu na kupoteza michezo miwili ikimaliza duru la kwanza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi.
Ndani ya michezo hiyo, Yanga Princess ilionekana kuwa na upungufu wa wachezaji wazuri eneo la ulinzi wa pembeni na kiungo mshambuliaji kutokana na waliokuwapo kutoonyesha ubora.
Mwanaspoti tulizungumza na Mratibu wa wananchi hao, Kibwana Matokeo ambaye alisema msimu huu wamejipanga kufanya marekebisho ya timu ikiwamo usajili wa maana.
“Bado tutatambulisha wachezaji wengine kama taratibu zitakamilika, kuna baadhi mambo ya usajili hayajakamilika, hivyo kila kitu kikiwa sawa mtajua,” alisema Matokeo.