Tukisherehekea miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), ukiwa na miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, umefanya mambo makubwa ya kupigiwa mfano kuwatoa wajasiriamali sehemu moja kwenda nyingine.
ZEEA ni taasisi ya Serikali ambayo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2022, ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo.
Miongoni mwa kazi kubwa zinazofanywa na taasisi hii ni kuwapatia mafunzo wajasiriamali, masoko, kuweka miundombinu ya biashara, kuwalea na kuwakuza wajasiriamali.
ZEEA ikiwa na miaka miwili ndani ya kipindi cha Utawala wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, kuna mafanikio lukuki, kubwa kuliko wameshatoa mikopo yenye thamani ya Sh34.9 bilioni.
Katika mikopo hiyo tayari wamewafikia wajasiriamali wanufaika 24,696 mpaka kufikia Desemba 2024. Kati ya hao, wanufaika 14,441 ni wanawake na 10,255 ni wanaume, kati ya hao 9,008 wamefikiwa kwa kuwapa elimu ya fedha, zikiwemo za utunzaji wa fedha, kuchakata na kukuza biashara zao.
Kwa upande wa elimu ya kulima mwani na kuusarifu (kuchakata) wanawake ni 7,319 na wanaume ni 2,186.
Pia, wameunganishwa na wajasiriamali na masoko ikiwa wanawake 445 na wanaume 173.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan anasema wamepunguza gharama ya upatikanaji wa alama ya ubora kwa kushirikiana na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) ambapo walisaini mkataba kupunguza kutoka kulipia Sh700,000 mpaka Sh50,000.
“Pia, tumetambua viwanda 30 ambavyo vinajihusisha na masuala ya utengenezaji wa sabuni, kwa sababu kuna soko kubwa la utalii, kuna hoteli zaidi ya 800, kwa hiyo ni soko kubwa, wajasiriamali wetu wataweza kupeleka sabuni na kujikuza kiuchumi,” anasema.
Kama hilo halitoshi, wakala umehama kutoka kwenye analogia kwenda kwenye dijitali, hivyo mpaka sasa kuna mifumo minne, mfumo wa utoaji wa mikopo, mfumo wa utoaji mafunzo na mfumo wa kuwaunganisha na masoko ya kidijitali.
“Tayari tumepata vibali kutoka Serikali Mtandao (Egav) chini ya usimamizi wa taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji Utendaji Serikalini (ZPDB) vya kupata mifumo.
“Wameweza kuondosha changamoto wakati wa utengenezaji wa mifumo na tumeshafanya majaribio, kwa hiyo hivi karibuni tutaanza kutoa mikopo kwa njia ya kidijitali,” alisema.
Mkurugenzi Burhan anasema mabadiliko ya kiteknolojia ni mabadiliko makubwa sana, kwani zipo taasisi kubwa zina muda mrefu lakini hazijafanikiwa kupata teknolojia, kwa hiyo “hilo najivunia hata kwangu mie ni faraja.”
Pia, ZEEA tumekuwa tunaandika miradi mingi ya kuwawezesha wajasiriamali na kwa sasa tumepata mradi mmoja wenye thamani ya Sh13 bilioni kupitia Benki ya Dunia na hivi karibuni tutaanza kuupata.
Upande wa pili, Mkurugenzi Burhan anasema ukiangalia kuwafikia wajasiriamali hao sio kazi ndogo, haya ni mafanikio makubwa, maanake wametatua changamoto kubwa za wajasiriamali.
Kadhalika, kuwafikia watu zaidi ya 10,000 kuwasomesha na kuwapa mafunzo na kuwatoa kwenye ujinga na kwenda kwenye werevu haya nayo ni mafanikio makubwa.
“Lakini tunapojenga ushirikiano na wadau katika sekta mbalimbali, kwa sasa tuna tamasha tunaita Fahari Yetu, tumefanya mwaka jana na mwaka huu tunafanya lingine ambalo litakuwa na namna yake, angalau kufanana na maonyesho ya Sabasaba.
Katika kuendeleza ujasiriamali kisiwani hapa, anasema baadaye Septemba 2025 wanatarajia kwenda nchini China katika ziara maalumu na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi na yale watakayoyakuta kule China watayaleta nchini kuwasaidia wajasiriamali hao.
Aina ya wajasiriamali wanaohudumiwa na ZEEA
Kuna wale ambao wanakuwa wanaanza hawana kitu chochote isipokuwa wana wazo tu (Startups), hawa wanapigwa msasa na ZEEA na kufikia sehemu fulani.
“Anayeanza kabisa, tuna kituo kinaitwa Zanzibar Technology and Business Incubation ambacho kinamlea na kumkuza kuanzia kwenye wazo, akitoka kwenye wazo anarasimisha kisha anatengeneza mfumo wa biashara anayoitaka, hivyo tunampa mkopo au ruzuku,” alisema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Burhan, kwa sasa kuna programu inaitwa Incubation Univesity Student ambayo wameanza na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) kisha baadaye watakwenda Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) na watakwenda kwenye vyuo vingine, lengo ni kuondoa mitazamo hasi ya kusoma kusubiri waje kuajiriwa, badala yake wafikirie kujiajiri.
Pia, kuna kundi la pili limeshaanza ambalo wanakuwa na changamoto tofauti, ikiwemo mitaji na mwingine unakuta ana bidhaa lakini hawana masoko, kwahiyo ZEEA inawaunganisha na masoko.
Kuna kundi lingine unakuta mtu ana fedha na soko analo lakini hakui, kumbe inakuwa hana elimu ya fedha, kwa hiyo hao nao wanapewa elimu ya fedha na ZEEA.
“Mwingine unakuta hana uwezo wa kutengeneza mifumo, kwa hiyo anakuja anasaidiwa, kila mmoja anakuwa anatatuliwa tatizo lake, mimi ninakuwa kama daktari kila mmoja anakuja na tatizo lake nalitatua kwa namna linavyokuwa linahitaji kutatuliwa,” anasema.
Hata hivyo, anasema kuna watu wakubwa (wafanyabiashara wakubwa) ambao nao wanatakiwa kuwezeshwa hata kama siyo elimu wala masoko, isipokuwa anatakiwa kupewa fursa.
“Kama mfanyabiashara mkubwa anaweza kutengeneza (Processing Centers), wajasiriamali wanaingia kisha yule ananunua bidhaa zao zote, kwa hiyo sisi tutamsaidia na kumpa eneo, hatumuachi mtu, kila mmoja anayehitaji kuwezeshwa anawezeshwa katika mfumo ambao utabadilisha maisha na kutengeneza ajira,” anasema.
Anasema kuna programu nyingi, zikiwemo za mikopo ambazo zipo nne; Kuna mkopo unaitwa Inuka kwa kushirikiana na CRDB, kuna mikopo inaitwa MSME kopa ambayo inafanywa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na kuna programu ya makundi maalumu maarufu 4,4,2 wanashirikiana na Benki ya Biashara (TCB) na mikopo ya vifaa vya nyuki.
Pia kuna programu ya mafunzo na programu za kiubunifu, na programu ya kuwafundisha watu namna ya processing, ICT na masuala ya utalii.
“Tunakuja na programu inaitwa uwezeshaji kijiweni bado haijaanza lakini hivi karibuni inategemea kuanza, kuna watu wengi wanakaa vijiweni sana, kwa hiyo tutataka kuwaondoa kwenye vijiwe,” anasisitiza.
Mkurugenzi huyo anasema mwaka 2025 wanataka kukamilisha ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa asilimia 100, “mpaka sasa tumeifanya kwa asilimia 80, kwa hiyo ndani ya miezi mitatu tunataka tuwe tumekamilisha na kupita ilani.
Katika mwaka huu pia watajitathmini kuona hatua zilizopigwa na wajasiriamali