Bavicha, Bazecha mguu sawa kuwapata viongozi wa kitaifa

Dar es Salaam. Ukweli kuhusu kina nani watakaopewa nafasi za kuyaongoza mabaraza ya wazee na vijana ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa nafasi za kitaifa, unatarajiwa kujulikana leo Jumatatu, Januari 13, 2025.

Hilo linatokana na kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Vijana (Bavicha) na Wazee (Bazecha) kumpata Mwenyekiti wa Taifa na Makamu wake Bara na Zanzibar.

Uchaguzi huo pia utahusisha Naibu Makatibu Wakuu Bara na Zanzibar, Mweka Hazina, na waenezi wa mabaraza hayo.

Mkutano wa uchaguzi wa Bavicha unafanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, huku wa Bazecha ukifanyika katika makao makuu ya Chadema, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema unapofanyika uchaguzi huo, wanachama wanapaswa kukumbuka kwamba kinachowaniwa ni zaidi ya nafasi za uongozi, bali kuunda mustakabali mzuri kwa chama hicho na Taifa.

Katika nafasi ya uenyekiti wa Bavicha, wanaogombea kumrithi John Pambalu ni Deogratius Mahinyila, Hamis Masud, na Shija Shibeshi.

Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, wagombea ni Vitus Nkuna, Necto Kitiga, Juma Ng’itu, Nice Sumari, na Mkolla Masoud.

Abdallah Rashid Haji ni mgombea pekee katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, huku Benjamin Nteje, Idrisa Rubibi, Dua Lyamzito, na Sheila Mchamba wakiwania nafasi ya Katibu Mkuu.

Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara inagombewa na Emanuela Kastuli na Revline Mbughi, huku Awena Nassor na Said Abdalla Hamis wakiwania upande wa Zanzibar.

Ni wagombea wawili pekee waliojitokeza kuwania uratibu wa uhamasishaji, ambao ni Felius Kinimi na Dedan Wangwe, na nafasi ya Mweka Hazina inawindwa na Badi Ibrahim, Michael Materu, na Rahima Abdallah.

Kwa upande wa wagombea wa Bazecha, Hashim Juma Issa anayetetea nafasi hiyo anakabiliana na Suzan Lyimo, ambaye ni makamu wake Bara.

Wengine kwenye nafasi hiyo ni John Mwambigija, Hugo Kimaryo, na Mwerchard Tiba.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Bara, amejitokeza Shaban Madede pekee, huku Makamu Mwenyekiti Zanzibar ikiwaniwa na Mohamed Ayoub Haji na Hamoud Said Mohamed.

Wanaogombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Bazecha ni Dk Leonard Mao, Hellen Kayanza, na Casmir Mabina, ambaye amewahi kuwa Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Bara, wanaowania ni Hamid Mfaligundi na Omary Mkama, huku upande wa Zanzibar ukiwakilishwa na Rajab Khamis Bakari, ambaye ni mgombea pekee, sawa na Mweka Hazina Florence Kasilima.

Akizungumzia uchaguzi huo kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ametaja siku hiyo kuwa muhimu wanapofanya uchaguzi wa mabaraza ya wazee na vijana.

Ametumia jukwaa hilo kuwapongeza wagombea wanaoshiriki, huku akisema kila mmoja ana thamani katika kupigania maono ya chama hicho.

“Katika safari yetu hii, hebu tukumbuke kwamba uchaguzi huu ni zaidi ya nafasi; ni kuhusu kuunda mustakabali mzuri kwa Chadema na kwa Taifa letu. Sote tuna jukumu la kuilinda taasisi yetu na kuhakikisha tunamaliza hatua hii tukiwa imara zaidi,” ameandika Mbowe.

Amewasihi wanachama na wafuasi wote kufuatilia mchakato huu wa kidemokrasia ndani ya chama hicho, huku akihimiza umoja katika kufanikisha mambo mbalimbali makubwa.

“Tunaposhirikiana, tunaweza kujenga Chadema yenye nguvu zaidi, kwa sababu yeyote atakayechaguliwa, Chadema imeshinda,” ameandika.

Hali ilivyo ukumbini Bavicha

Katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, unakofanyikia uchaguzi wa Bavicha, hadi saa 10:10 asubuhi ni idadi ndogo ya wajumbe waliokwishafika.

Lakini, wakati huo tayari maandalizi yalishakamilika kwa maana ya nakshi za nje na ndani ya ukumbi na mpangilio wa maeneo ya kukaa kwa wajumbe.

Ulinzi pia umeimarishwa na vijana wa chama hicho waliovalia mavazi meusi, huku fulana zenye nembo ya Bavicha zikiwa ndilo vazi lililovaliwa na wengi waliofika ukumbini hapo.

Katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, kunakofanyika uchaguzi wa Bazecha, wajumbe wa mkutano huo wamekaa makundi makundi wakijinadi huku wakisubiri kupewa utaratibu rasmi.

Wajumbe hao kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, wengi wao wana mabegi mgongoni ikiwa ni ishara ya safari ndefu waliyoifanya kufika Dar es Salaam kwa ajili ya mageuzi ya kutumia haki yao ya kikatiba kufanya uamuzi.

Kila mjumbe anayewasili katika ukumbi wa chama hicho hupaswa kuingia ndani ya ukumbi punde baada ya kujiandikisha na kupewa kitambulisho.

Utambulisho wa kila mjumbe na mgombea umewekwa picha yenye kumuonyesha kama mjumbe halali wa uchaguzi huo.

Pamoja na vitambulisho wanavyovaa shingoni, wajumbe hao wanatambuliwa pia kwa fulana zenye nembo za chama pamoja na suruali na shati la kaki.

Imeandikwa na Juma Issihaka, Baraka Loshilaa, Tuzo Mapunda, na Bakari Kiango

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea kwenye uchaguzi.

Related Posts