Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ameendelea kusota rumande kwa siku 746 kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili; kujipatia Sh5.1bilioni 5.1 kwa udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, kesi inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Inadaiwa mshtakiwa alijipatia fedha hizo kutoka kwenye Saccos ya Jatu kwa kudai fedha hizo zingetumika kupanda mazao ili kuzalisha faida zaidi, akijua madai hayo si ya kweli.
Hadi leo, Jumatatu, Januari 13, 2025, Gasaya amekuwa gerezani kwa siku 746, sawa na miaka miwili na siku 15, kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Kesi hiyo iliitwa leo kwa ajili ya kutajwa, na wakili wa Serikali, Roida Mwakamele, aliieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, kwamba upelelezi bado unaendelea na akaomba tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hata hivyo, mshtakiwa hakuwasilishwa mahakamani leo kwa sababu mahabusu wa gereza la Keko hawakupelekwa mahakamani.
Hakimu Mwankuga ameahirisha kesi hadi Januari 27, 2025, kwa ajili ya kutajwa. Gasaya anaendelea kushikiliwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha, ambalo halina dhamana kisheria.
Gasaya alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 29, 2022, na kusomewa mashtaka mawili ya uhujumu uchumi; kujipatia fedha kwa udanganyifu na kutakatisha fedha.
Tangu siku hiyo, amekuwa rumande kwa siku 746, sawa na dakika 1,078,560 au sekunde 64,713,600, kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika na shtaka la kutakatisha fedha, ambalo halina dhamana.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari mosi, 2020, na Desemba 31, 2021, jijini Dar es Salaam, alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka kwenye Saccos ya Jatu kwa udanganyifu, akidai kuwa fedha hizo zingetumika kupanda mazao na kuzalisha faida.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha, ambapo Gasaya anadaiwa kati ya Januari 1, 2020, na Desemba 31, 2021, akiwa Mtendaji Mkuu wa Jatu PLC, alihamisha Sh5,139,865,733 kutoka akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya NMB tawi la Temeke kwenda akaunti ya Jatu PLC katika Benki ya NMB tawi la Temeke, akijua fedha hizo zilitokana na kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu.