BoT yanunua dhahabu ya Sh400 bilioni kwa miezi mitatu

Geita. Motisha inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa wafanyabiashara wa dhahabu, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa dhahabu kwa bei ya soko la dunia, kuondolewa kwa tozo ya ukaguzi na punguzo la tozo ya asilimia mbili ya mrabaha, imeisaidia benki hiyo kukusanya tani mbili za dhahabu zenye thamani ya Sh400 bilioni kuanzia Oktoba 2024.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuongeza thamani kwa wanawake wachimbaji yaliyotolewa na Kiwanda cha Kuongeza Thamani ya Dhahabu (GGR) kwa kushirikiana na BoT, Ofisa kutoka kitengo kinachosimamia fedha za kigeni kutoka BoT, Joshua Mganga, amesema motisha hiyo imeongeza mwamko mkubwa kutoka kwa wachimbaji kuiuzia benki hiyo dhahabu, ikilinganishwa na mauzo ya mwaka 2023.

Amesema lengo la Serikali kununua dhahabu ni ili kuongeza fedha za kigeni, kuimarisha uchumi na kuwasaidia wachimbaji wa ndani kuimarisha mitaji yao.

Meneja wa Wakala wa Huduma za Serikali kutoka BoT, Sadiki Nyanzuwa, amesema awali wachimbaji wengi walikuwa hawakopesheki kutokana na kukosa dhamana, lakini sasa Serikali imeingilia kati kwa kuweka nguvu ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu utakaosaidia nchi kupata fedha nyingi.

“Wachimbaji wengi hawakopesheki kutokana na kukosa dhamana, na sasa Serikali imeamua kuingilia kati. Kwa sasa hivi, Serikali inafanya jitihada za kuongeza uzalishaji ili tuweze kupata fedha nyingi. Imenunuliwa mitambo, na kwa kutambua uchimbaji wa dhahabu ni biashara kama biashara nyingine, BoT imeamua kununua dhahabu yenyewe na kuwadhamini wachimbaji kwa niaba ya Serikali,” amesema Nyanzuwa.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zilizopo nchini.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, wanawake 1,000 wamepatiwa leseni za uchimbaji na sasa wapo kwenye mchakato wa kutoa leseni zaidi ya 2,000 katika eneo la Kigosi, ambalo awali lilikuwa hifadhi ya misitu.

“Maombi ni mengi, leseni 2,300 lakini maombi ni zaidi ya 4,000. Hata hivyo, tumewaelekeza wachimbaji kwa eneo lililotengwa kwa ajili yao na leseni nyingine zaidi ya 4,000 tayari. Nimewapa maelekezo ya kutangaza leseni hizo ili wale waliokosa waweze kuomba,” amesema Shigella.

Ofisa Madini Mkoa wa Geita, Samuel Shoo, amesema hadi sasa leseni 355 za uchimbaji zimetolewa kwa wanawake. Amesema tofauti na miaka ya nyuma ambapo wanawake walikuwa wakijishughulisha na kazi ndogo ndogo, sasa wamekuwa na uthubutu na wanajiwekeza kwenye uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Wanawake (Tawoma), Salma Ernest, amesema mafunzo ya kuongeza thamani yaliyotolewa kwa wachimbaji wanawake yalilenga kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini.

Ernest amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo katika teknolojia ya uchimbaji wa kisasa, uchakataji wa madini na mbinu za kuzingatia kanuni za usalama na mazingira, huku wakitakiwa kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa leseni.

Meneja wa tawi la Benki ya Azania Mkoa wa Geita, Rhoda Baluya, amesema wao kama taasisi za kibenki wameshiriki mafunzo hayo kuwaeleza wanawake wachimbaji kuhusu fursa za mikopo zinazopatikana kutokana na BoT kuwadhamini.

“Kwa hiyo, suala la kukopesha kina mama itakuwa rahisi kwa sababu shughuli inayolipa mkopo ipo na oimekubali kuwadhamini. Tunawapa elimu ya namna ya kutunza nyaraka na umuhimu wa kutumia huduma za kibenki,” amesema Baluya.

Ofisa Mikopo CRDB tawi la Dhahabu, amesema benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wanawake kupitia programu ya Imbeju inayohusu kina mama na vijana. Hadi sasa benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh34 bilioni kwa wachimbaji wa dhahabu.

Related Posts