Mwanza. Baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyegezi jijini Mwanza wameziomba mamlaka husika kuwaondoa wapigadebe katika Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi kwa madai kuwa uwepo wao unachangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, ikiwemo wizi.
Ombi hilo limetolewa leo Jumatatu, Januari 13, 2025, katika kikao cha CCM Kata ya Nyegezi kilichokuwa kikijadili changamoto za ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Mtaa wa California, Fadhili Nassoro, amesema wapigadebe hao wanahusishwa na vitendo vya uhalifu, ambavyo vimekuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na abiria wanaofika stendi hapo, hasa nyakati za usiku.
“Vitendo vya uhalifu vimeongezeka kwa kiasi kikubwa na mara nyingi vinahusishwa na vijana walioko kwenye vituo vya mabasi maarufu kama wapigadebe. Wengi wao wamekuwa wakiwaibia abiria mali zao. Tunaomba mamlaka ziwachukulie hatua na kuwaondoa kabisa katika eneo hili,” amesema Fadhili.
Aidha, mjumbe wa kikao hicho, Phidelis Kaombwe, amependekeza kuondolewa kwa vituo vya kubebea na kushushia abiria ambavyo vimezagaa katika eneo hilo, akisema vinatumiwa kama maficho ya wapigadebe hao.
“Serikali haitambui kazi ya upiga debe kwa sababu haina leseni rasmi. Naomba tutengeneze utaratibu maalumu wa kuwapa jezi au vitambulisho ili wale wanaofanya kazi kwa halali watambulike, huku tukidhibiti wale wanaojihusisha na uhalifu,” amesema Kaombwe.
Hata hivyo, mmoja wa wapigadebe wa stendi hiyo, Majaliwa Abdallah, amekanusha madai hayo akisema wanaitumia kazi hiyo kujipatia kipato halali kwa ajili ya familia zao.
“Kabla ya kutuondoa hapa, tunaomba Serikali itutengee utaratibu mzuri wa kututambua rasmi kama sehemu ya mfumo wa shughuli zinazofanyika stendi hii. Tunajitafutia riziki kwa njia halali, siyo wote tunaohusika na vitendo vya uhalifu,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, amesema ofisi yake inasubiri mapendekezo rasmi kutoka kwa viongozi wa CCM kuhusu suala hilo ili litafutiwe suluhisho lisilomuathiri mtu yeyote.
“Hili ni suala jipya kwa ofisi yangu. Nitasubiri kupokea barua ya maelezo na mapendekezo yao, kisha tutalifanyia kazi kupitia kikao maalum,” amesema Kibamba.
Januari 10, mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, akitoa taarifa ya hali ya usalama mkoani humo alisisitiza kuwa hali ya usalama mkoani Mwanza ni shwari, huku akiahidi kuwa wale watakaobainika kufanya uhalifu hawatovumiliwa.