Chato kunufaika na mazao ya misitu miaka 10 ijayo

Mufindi. Wananchi wa Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, wametakiwa kujiandaa kufurahia matokeo ya mazao ya misitu kupitia shamba la miti la Silayo lililopo wilayani humo, huku Serikali ikilenga kuimarisha uchumi wa eneo hilo.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 13, 2025, baada ya ziara ya mafunzo katika Shamba la Miti la Sao Hill, Wilaya ya Mufindi, Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Louis Bura, amesema shamba la miti la Silayo litakuwa chanzo kikubwa cha maendeleo kwa Chato katika miaka 10 ijayo.

“Kwa sasa naiona Chato mpya itakayokuwa na mageuzi makubwa kutokana na mazao ya misitu. Tutakuwa na mbao, viwanda, na uvunaji wa asali, na hayo yote yatachangia kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Bura.

Amebainisha kuwa Chato ina jumla ya hekta 4,800 za misitu ya kupanda, huku matarajio yakiwa ni kufikia hekta 62,000. Pia, maeneo maalumu yameshatengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na maegesho ya malori kwa ajili ya kupakia mbao.

“Biashara yetu itajikita zaidi katika soko la ndani, hasa Mkoa wa Mwanza, na tutalenga pia masoko ya nchi jirani kama Kenya na Uganda,” ameongeza.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa, aliwakaribisha viongozi hao kutoka Chato kwa ziara hiyo na kuwapongeza kwa jitihada zao za kujifunza kuhusu uhifadhi wa misitu na usimamizi wa mazingira.

“Wilaya yetu imepiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mazingira na ukusanyaji wa mapato, jambo ambalo limewezeshwa na uwepo wa shamba la miti la Serikali, Sao Hill,” amesema Dk Salekwa.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, Teddy Yoram, ameeleza kuwa uhusiano mzuri kati ya shamba na jamii inayozunguka umekuwa nguzo muhimu kwa mafanikio yao. Utoaji wa ajira kwa wananchi wa maeneo jirani umeimarisha mshikamano na kusaidia uhifadhi wa mazingira.

Stella Masabile, Diwani wa Kata ya Kachwamba wilayani Chato, amesema ziara hiyo imewafungua macho kuhusu faida za rasilimali za misitu.

“Ziara hii imenipa motisha kuanza kupanda miti kwenye hekari tano nyumbani kwangu. Baada ya miaka 15, miti hiyo itabadilisha maisha yangu. Nitahamasisha wananchi pia kupanda miti ili kunufaika na rasilimali hii,” amesema Masabile.

Related Posts