Cheche amrithi Kijuso Cosmopolitan | Mwanaspoti

MABINGWA wa zamani wa soka nchini, Cosmopolitan imefikia uamuzi wa kumpa mkataba wa miezi sita aliyekuwa kocha wa Azam FC, Idd Nassor ‘Cheche’, ikiwa ni wiki moja tu tangu wamtimue Mohamed Kijuso kutokana na mwenendo mbaya ambao timu hiyo imekuwa nao msimu huu.

Cosmo iliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Bara mwaka 1967 na inapambana kurejea katika ligi hiyo inayoisotea tangu mwaka 1970, ikiwa ni zaidi ya miaka 50 sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Cheche alikiri kujiunga na timu hiyo huku akiweka wazi ana kazi kubwa ya kufanya ili kikosi hicho kilete ushindani, ingawa sio mgeni wa Ligi ya Championship hivyo anachoomba ni ushirikiano.

“Timu haiko mahali pazuri na nimeichukua katika kipindi kigumu lakini mimi kama kocha jukumu langu ni kuitoa sehemu moja kwenda nyingine, nashukuru viongozi wameniahidi kunipa sapoti ya kutosha hivyo na mimi nawaahidi kutowaangusha,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Pan Africans, aliongeza jambo kubwa atakaloanza nalo ni kutengeneza nidhamu kuanzia ya wachezaji wenyewe, ushirikiano na kuunda pia mikakati mizuri ambayo itawarahisishia utendaji wa kazi baina yao ili wafanye vyema.

Kijuso msimu huu hadi anaondoka ndani ya kikosi hicho alikiongoza katika michezo 14 ya Ligi ya Championship, ambapo kati ya hiyo alishinda miwili, sare miwili na kupoteza 10, akikiacha kikiwa katika nafasi ya 13, kwenye msimamo na pointi zake nane.

Related Posts