Haji Mnoga akipiga dakika 58 dhidi ya Man City

LICHA ya chama la beki Mtanzania, Haji Mnoga wa Salford City ya Uingereza kupokea kichapo cha mabao 8-0 dhidi ya Manchester City, nyota huyo alianza na kukipiga kwa dakika 58.

Salford juzi ilikuwa kwenye Uwanja wa Etihad jijini Manchester kuvaana na Man City katika mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la FA.

Beki huyo wa kulia alianza kwenye kikosi hicho akicheza kwa dakika 58 akifanyiwa mabadiliko baada ya kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Jon Taylor.

Licha ya ubora wa Man City lakini Mtanzania huyo alionyesha ukomavu mkubwa kuhakikisha anaendana na kasi ya mabingwa hao mara nne mfululizo wa Ligi Kuu England.

Hata hivyo, Mnoga alifanyiwa mabadiliko baada ya kiungo wa Man City, Jack Grealish kumchezea rafu ya mguu iliyomfanya ashindwe kuendelea na mchezo.

Ukiwa mchezo wa kihistoria kwa nyota huyo kuwa Mtanzania mwingine aliyecheza dhidi ya Man City baada ya Mbwana Samatta aliyewakabili vijana wa Pep Guardiola katika Kombe la Carabao kwenye Uwanja wa Wembley wakilala 2-1, huku Samatta akifunga bao moja la Aston Villa.

Hadi sasa Mnoga amecheza mechi 26 za mashindano yote, timu yake ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi na pointi 42 kwenye michezo 24 ushindi 12, sare sita na kupoteza sita.

Kabla ya kujiunga na klabu hiyo ya Ligi Daraja la Tatu msimu huu, Mnoga alipita Portsmouth, Aldershot Town na Gillingham.

Related Posts