Kalambo yaanzisha utalii wa nyuki, kuimarisha afya na uchumi

Rukwa. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, umeanzisha utalii wa nyuki, lengo likiwa ni kutoa fursa kwa watalii kujifunza ufugaji wa nyuki.

Utalii huo unatoa nafasi kwa watalii kujionea shughuli za ufugaji nyuki katika hifadhi ya mazingira asilia Kalambo, ikiwa ni pamoja na kupata huduma ya kudungishwa nyuki mwilini, inayochochea na kuimarisha kinga za mwili.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 13, 2025, wakati wa uzinduzi wa utalii huo, askari wa uhifadhi wa TFS Kalambo, Daniel Dotto, amesema kuwa Serikali imeanzisha shamba maalumu kwa ajili ya ufugaji nyuki na kutoa mizinga 500 yenye thamani ya Sh150 milioni. Mizinga hiyo itawawezesha watalii kujifunza namna bora ya ufugaji nyuki kisasa.

Dotto amesema, “Mtalii ataweza kujionea mazingira halisi ya ufugaji nyuki na mazingira ya ikolojia ya msitu huu, ikiwa ni pamoja na kutembelea maporomoko ya maji ya Mto Kalambo, ambayo ni ya pili kwa urefu Afrika, yenye mita 235 kutoka kwenye chanzo chake.”

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Ibrahim Mkiwa, amesema kuwa uwepo wa utalii huo utaongeza mapato ya Serikali, pamoja na watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, ambapo idadi ya watalii kwa sasa inakadiriwa kuwa 1,000 kwa mwaka.

Amesema pia kuwa wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kujifunza namna bora ya kutengeneza mizinga na ufugaji nyuki kisasa.

Mkiwa amesisitiza kuwa endapo mtalii atadungwa sindano ya nyuki, ataimarisha afya yake, kwani nyuki wana uwezo wa kuongeza kinga ya mwili.

Uanzishwaji wa utalii huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha wawekezaji na watalii kutembelea vivutio vya ndani.

Mhifadhi huyo amesema kuwa ni muhimu kubadilisha mtazamo kwamba watalii lazima watoke nje ya nchi, kwani hata wazawa wanapaswa kutembelea vivutio mbalimbali katika maeneo yao.

“Imekuwa desturi kwamba watalii lazima watoke nje ya nchi, jambo ambalo sio kweli. Niwatake wananchi wa Kalambo kutembelea maporomoko ya maji na kujifunza ufugaji nyuki wa kisasa,” amesema Mkiwa.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kufanya utalii wa kudungwa sindano za nyuki, akiwemo Stanislaus Wangao, wameeleza kuridhika na huduma hiyo, wakisema kuwa kumekuwa na mabadiliko chanya katika afya zao.

Wangao amesema, “Tangu kuanzishwa kwa utalii huu, na kuambiwa kuwa ukidungwa na nyuki, utaimarika kiafya, umekuwa ni kivutio kikubwa na utaongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.”

Utalii huo wa nyuki unatarajiwa kuwa chanzo kipya cha mapato kwa wananchi na Serikali, na kusaidia kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na afya bora.

Related Posts