Dodoma. Kesi ya mauaji ya Grayson Kanyenye (6) inayowakabili Kelvin Joshua (27), dereva bodaboda na Tumaini Msangi (28), bondia, imeahirishwa hadi Januari 27, 2025 kutokana na upelelezi kutokamilika.
Washtakiwa hao walifikishwa leo Jumatatu, Januari 13, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, mbele ya Hakimu Mkazi, Charles Eligy, kesi hiyo ilipotajwa.
Hata hivyo, wakili wa Serikali mwandamizi, Patricia Mkina, ameiambia mahakama kuwa upelelezi wake haujakamilika, hivyo kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa.
“Mheshimiwa Hakimu, shauri hili liko mbele yako kwa ajili ya kutajwa na kwa sababu upelelezi bado unaendelea na hakimu anayesikiliza shauri hili hayupo, tunaomba kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Patricia.
Baada ya ombi hilo, Hakimu Eligy pamoja na wakili anayemwakilisha mshtakiwa wa pili, Msangi, Luciana Nyondo, waliridhia ombi hilo na kesi kuahirishwa hadi Januari 27, mwaka huu.
Kelvin na Tumaini wanashtakiwa kwa kosa la mauaji ya mtoto Grayson Kanyenye (6) yaliyotokea Desemba 25, 2024, nyumbani kwa Hamis Mpeta, eneo la Ilazo Extension, aliyekuwa na uhusiano na mama mzazi wa mtoto huyo, Zainabu Shaban (Jojo).
Jojo ambaye ni mfanyabiashara, wakati anaondoka alimwacha mtoto huyo mikononi mwa dereva bodaboda Joshua, baada ya kurudi asubuhi kutoka matembezini, alikuta ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kujeruhiwa maeneo ya shingoni.