Dodoma. Kesi ya mauaji ya mtoto Grayson Kanyenye (6) inayowakabili dereva bodaboda Kelvin Joshua na bondia Tumaini Msangi inatarajiwa kusomwa tena leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.
Watuhumiwa hao wawili wanakabiliwa na shtaka la kumuua kwa kukusudia mtoto huyo Desemba 25, 2024, eneo la Ilazo Extension, Jijini Dodoma.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 30, 2024, na kusomewa mashtaka yao na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Patricia Mkina, mbele ya Hakimu Mkazi Denis Mpelembwa. Hawakutakiwa kujibu kitu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji.
Washtakiwa hao walirudishwa rumande kwa sababu kesi inayowakabili haina dhamana.
Mtoto Grayson alikutwa ameuawa na watu wasiojulikana Desemba 25, 2024, eneo la Ilazo Extension, Jijini Dodoma, nyumbani kwa Hamis Mpeta, aliyekuwa na uhusiano na mama mzazi wa mtoto huyo, Zainabu Shaban maarufu Jojo, ambao walimwacha chini ya uangalizi wa dereva bodaboda Joshua.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, George Katabazi wakati huo ilieleza kuwa baada ya mama mzazi kufika nyumbani asubuhi ya Desemba 25, 2024, walikuta mtoto huyo ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kujeruhiwa maeneo ya shingoni.