KIUNGO wa zamani wa Mbeya City, Yanga na Namungo, Raphael Daudi Loth amekamilisha uhamisho wake kwa mkopo wa miezi sita kuitumikia Coastal Union.
Awali, Daud alikuwa akicheza kwa mkopo Namungo FC akijiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu baada ya kukaa kwa takriban miezi sita, alirejea Singida Black Stars iliyoamua kumpeleka Coastal Union.
Kiungo huyo awali alikuwa anaripotiwa kutua Fountain Gate lakini mambo yamebadilika na sasa ataitumikia Coastal Union kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alithibitisha taarifa za mchezaji huyo kwenda Coastal Union kwa mkopo huku akiweka wazi kuwa taarifa kwa kina zitatolewa wakati wowote na klabu hiyo.
“Ni kweli Daudi anaenda Coastal Union baada ya uongozi wa timu hiyo kutuma barua ya maombi kumuhitaji na kila kitu kimekamilika, kilichobaki ni taarifa rasmi kutolewa na klabu na kuwekwa kwenye mitandao yetu ya kijamii,” alisema Massanza.
Daudi ambaye ameshawahi kukipiga Yanga, anakwenda kuitumikia Coastal Union inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 16 ikifanikiwa kukusanya pointi 18, hivyo ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha anashirikiana na wenzake kuipambania timu hiyo ifikie malengo na kuepuka kushuka daraja.