Moshi. Mafundi rangi na ujenzi mkoani Kilimanjaro wameamua kujitafuta ili kukabiliana na changamoto za kitaaluma, kimazingira, na kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia weledi unaohusiana na shughuli zao.
Mafundi hao, ambao sasa wanaunda umoja wao kupitia chama cha Mafundi Rangi na Ujenzi Mkoa wa Kilimanjaro (Chamaruki), wamekusudia kutumia fursa mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha shughuli zao za kitaaluma.
Akizungumza na mafundi hao katika mkutano mkuu wa kwanza wa chama hicho, uliofanyika mjini Moshi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Shaban Mchovu, amewataka kuwa waaminifu na kulinda nidhamu ya kazi ili wanufaike na fursa za ujenzi zilizopo ndani ya Serikali na taasisi binafsi.
Mchovu amesisitiza kuwa nidhamu, upeo wa kuziendea fursa, hasa kupitia mitandao na majukwaa mbalimbali, ni jambo muhimu kwa mafundi ili kufanikisha kazi zao na kujikwamua kiuchumi.
Amewahimiza mafundi kuwa na umoja na kuhamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye fursa za ujenzi. Ameahidi kuwa Serikali ya wilaya hiyo itaunga mkono juhudi zao na kuhakikisha wanapata ofisi.
“Nasisitiza nidhamu ya kazi, matumizi sahihi ya mtandao, na kuhamasisha wanawake kujiunga katika umoja huu. Mnapokuwa wamoja, mnaweza kutengeneza mtandao mzuri utakaowasaidia kusonga mbele,” amesema Mchovu.
Aidha, Mchovu ameongeza kuwa mafundi wanapaswa kuwa na programu za simu (application) ili mtu anayetaka huduma za ujenzi aombe kupitia hiyo na fundi aje kufanya kazi.
Kwa upande wake, Katibu wa mpito wa chama hicho, Casmiry John, ameeleza lengo la kuanzisha chama hiki ni kutengeneza thamani ya mafundi katika jamii na kuziendea fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi kupitia umoja wao.
Amesisitiza kuwa msingi wa chama ni kuondoa dhana potofu iliyojengeka katika jamii, ambapo mafundi rangi na ujenzi mara nyingi hutazamwa kama watu waliokosa kazi za kufanya.
John pia ameomba Serikali kuwatazama mafundi hao na kuwapa kazi pindi zinapotokea, ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuchochea ukuaji wa maendeleo katika jamii.
Meneja wa Benki ya Azania Mkoa wa Kilimanjaro, Yusuf Lenga, amesema mafundi ni sehemu muhimu katika ujenzi wa jamii, na taasisi ya kifedha iko tayari kushirikiana nao kupitia umoja huo, ikiwemo kutoa elimu ya kifedha na mikopo yenye riba nafuu ili kusaidia mafundi kufikia malengo yao.
Baadhi ya mafundi wanaounda umoja huo wameeleza matumaini yao na umuhimu wa kuwa na chama hicho katika kufikia fursa zilizopo. Mkutano huo pia umehudhuriwa na wafanyabiashara na wadau mbalimbali kutoka sekta ya ujenzi, ambapo wajumbe walipitisha rasimu ya katiba yao na kujadili taarifa ya mapato na matumizi tangu kuanzishwa kwa chama hicho.