Unguja. Mamalishe wa Soko la Kinyasini, lililopo Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamelalamikia kukosa huduma ya choo, jambo linalowalazimu kufungiana kanga kujiziba wanapokwenda kujisitiri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 13, 2025, Semeni Salumu, mmoja wa mamalishe hao, amesema hali hiyo inawasikitisha kwa kuwa soko hilo linatakiwa kuwa na vyoo kwa ajili ya huduma za kibinadamu.
“Sisi wanawake tunafanya kazi katika mazingira magumu. Mtu anapokutana na shida au haja yoyote, tunalazimika kusaidiana kwa kuzibiana kanga, kinyume na hapo hatuna sehemu ya kujistiri,” amesema Semeni.
Amesema biashara ya mamalishe inahitaji usafi mkubwa ili kuepuka maradhi, lakini kukosa huduma ya vyoo katika soko hilo ni jambo la hatari.
Kwa upande wake, Fatma Nurdin ambaye naye ni mjasiriamali amesema wameshapeleka malalamiko yao kuhusu ukosefu wa vyoo katika soko hilo, lakini mpaka sasa hawajapata ufumbuzi.
Pia amesema changamoto nyingine katika soko hilo ni kukosa eneo maalumu la kupikia, hivyo kupika uwanjani jua na mvua kuendeleza biashara yao.
Amina Issa ameeleza kuwa wakati mwingine wanalazimika kutumia choo cha wanaume ambacho mlango wake haufungi. Amesisitiza kuwa wanawake wanahitaji sehemu ya faragha kwa ajili ya kujistiri, hivyo kuiomba uongozi wa soko kuzingatia jambo hilo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini A, Maryam Said Khamis, amekiri kuwapo kwa changamoto hiyo na kuahidi kuitafutia ufumbuzi. Amesema wajasiriamali hao walifika kwake na kutoa malalamiko yao, na baada ya kuwasikiliza aliwaita Manispaa ili kufafanua suala la ukosefu wa choo katika soko hilo.
Kiongozi huyo amefafanua kuwa mamalishe walikabidhiwa funguo ya choo kimoja, lakini walikuwa na changamoto ya kusafisha choo hicho, na hivyo kuwa sababu ya kupokonywa funguo zao.
“Mazingira ya kutoa huduma za chakula lazima yazingatie usafi, kwani bila usafi hakuna mtu atakayenunua bidhaa yako,” amesema.
Katibu tawala huyo ameahidi kushirikiana na mamalishe hao, kuandikiana makubaliano na kuhakikisha wanapata huduma ya choo na sehemu za kupikia kama ilivyohitajika.