Maria Sarungi asimulia namna alivyotekwa Kenya

Nairobi.  Mwanaharakati na mhariri wa kujitegemea, Maria Sarungi amedai  kuwa, watu wanne walimteka jana eneo la Kilimani jijini Nairobi, Kenya.

Taarifa za madai ya kutekwa kwa Maria zilianza kusambaa jana jioni kwenye mitandao ya kijamii, baada ya Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu, Amnesty International, kuchapisha taarifa kuhusu tukio hilo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter).

“Maria Sarungi Tsehai, mhariri huru wa vyombo vya habari nchini Tanzania na mtetezi wa haki za binadamu, ametekwa nyara na watu watatu wenye silaha katika eneo la Chaka, Kilimani jijini Nairobi,” inasema taarifa hiyo ya Amnesty International.

Akisimulia leo mbele ya waandishi wa habari jijini Nairobi, Maria amedai kuwa,  kati ya watu wanne waliomteka, mmoja alikuwa akipokea maelekezo kutoka kwa mtu aliyemtaja kama ‘bosi.’

“Nilitekwa na watu wanne, watatu walishuka kwenye gari na mmoja alikuwa amenishika muda wote, nahisi alipewa jukumu hilo. Mmoja ambaye alikaa mbele pamoja na dereva, nahisi ndiye alipewa maelekezo au alikuwa anapokea maelekezo. Huyu alikuwa mtu pekee aliyekuwa akizungumza Kiswahili kwenye gari,” amedai Maria.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa na watekaji hao, Maria amedai kuwa, walitaka kufahamu anajishughulisha na kitu gani jijini Nairobi.

“Niliulizwa kama nina mume, niliulizwa pia nafanya nini. Nikawajibu, ‘kabla hamjaniteka, mlikuwa mnajua mimi nafanya nini?’ Walikuwa wamevaa maski, lakini sauti zao zilinifanya nijue kuwa ni vijana,” amedai Maria.

Kuhusu masharti ya kuachiwa kwake, Maria amedai kuwa, baada ya kuachiwa juzi usiku, watekaji walimtaka asizungumze chochote na mtu yeyote kuhusu tukio hilo.

 “Walivyoniachia ilikuwa usiku, nakumbuka waliniteka kati ya saa tisa alasiri na walivyoniachia, waliniambia nisiongee na yeyote na nisiseme chochote. Ninachokumbuka, walitaka simu yangu na walikuwa wanazunguka na mimi huku wakisema wanamsubiri bosi wao” Nikawauliza, “kumbe mna bosi?,” walikasirika kwa kuhisi nimeanza kujua mipango yao.

 “Nawashukuru vyombo vya habari kwa kupaza sauti na watu, wanasiasa mbalimbali kwa kupaza sauti, pia, nawashukuru mabalozi na Serikali za Umoja wa Ulaya na wanaharakati mbalimbali. Maana sauti zao ziliwafanya watekaji wasite kuendelea na mipango yao,” amedai  Maria.

Polisi Kenya wametafutwa kuzungumzia madai hayo lakini hawakupatikana.

Related Posts