Mbeya. Mikoa ya Mbeya na Songwe iko mbioni kunufaika na huduma za mawasiliano baada ya Serikali kuanza ujenzi wa mkongo wa Taifa katika Kata ya Makongorosi, Wilaya ya Chunya.
Mradi huo utaanza kutumika Aprili mwaka huu, baada ya kukamilisha ufungaji wa waya wenye urefu wa kilometa 10 katika eneo hilo.
Wilaya ya Chunya ni miongoni mwa Wilaya 139 nchini zitakazofikiwa na uwekezaji huo, unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia na Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Januari 13, 2025, baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, amesema: “Wilaya ya Chunya katika Mkoa wa Mbeya ni moja ya Wilaya 139 nchini ambazo zitapitiwa na kituo cha mkongo wa Taifa. Lengo la Serikali ni kufikisha huduma za mawasiliano hadi maeneo yasiyofikika.”
Amesisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya vituo vya mkongo wa Taifa, kwenye maeneo ya nchi kavu na baharini.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kutarahisisha upatikanaji wa mawasiliano na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuri kwa watendaji wa Serikali.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhandisi Mahundi amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kituo hicho, huku akitoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili ilete tija kubwa kwa taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga, amesema uwekezaji wa ujenzi wa kituo hicho ni fursa muhimu kwa wananchi, kwani utasaidia kupunguza changamoto za mawasiliano zilizokuwa zikiwakumba baadhi ya maeneo.
“Ujenzi wa kituo cha mkongo wa Taifa katika Kata ya Makongorosi, Wilaya ya Chunya, unakwenda kuwa suluhisho la changamoto ya ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali, kutokana na ukosefu wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo,” amesema Batenga.
Batenga amewataka wananchi kuwa mabalozi wa kutunza na kulinda miundombinu hiyo ili kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.
Meneja wa Shirika la TTCL Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Mujuni Kyarusmzi, amefafanua kuwa mkongo wa Taifa utaunganisha Mikoa ya Mbeya na Songwe kupitia Wilaya ya Songwe.
Amesema utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho umefikia hatua nzuri na matarajio ni kwamba kitaanza kutumika Aprili mwaka huu, baada ya kukamilisha ufungaji wa miundombinu ya waya katika eneo lenye urefu wa kilometa 10.
Mchimbaji mdogo wa madini katika Kata ya Makongorosi, Joel Mussa, amesema uwekezaji huu wa Serikali unakwenda kuwa suluhisho kubwa kwao katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kupitia wizara husika kwa kufikisha huduma za mawasiliano, jambo ambalo litaongeza mapato ya serikali na kuchochea shughuli za kiuchumi,” amesema Mussa.