SIMBA Ubaya Ubwela. Wekundu hao wa Msimbazi wameandika historia nyingine kwa kufuzu robo fainali ya michuano ya CAF ikiwa ni mara ya sita katika misimu saba iliyoshiriki michuano hiyo tangu 2018-2019 baada ya kulazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola.
Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 10 na kujihakikishia kusonga mbele nyuma ya CS Constantine itakayokutana nayo wikiendi hii ili kuamua nani awe kileleni na yupo amalize wa pili.
Constantine imefikisha pointi 12 baada ya kuishindilia CS Sfaxien kwa mabao 3-0.
Katika mchezo huo wa Kundi A uliopigwa, Uwanja wa Taifa wa Novemba 11, uliopo Talatona, jirani na Jiji la Luanda, wenyeji ilitangulia kwa bao la dakika ya 13 lililofungwa na Abednego Keoikantse.
Bao hilo lilitokana na makosa yaliyofanya na beki wa Simba, Che Malone Fondoh kurudisha mpira nyuma kimakosa na kumkuta mfungaji huyo.
Hata hivyo kipindi cha pili Simba ilirejesha bao hilo, dakika ya 69, kupitia Leonel Ateba baada ya kupokea pasi nzuri ya beki wa kulia, Shomari Kapombe na kuupiga mpira uliomshinda kipa wa Bravos, Okiemute Odah.
Kikosi hicho cha Kocha, Fadlu Davids kiliingia katika mchezo huo kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam bao 1-0, la penalti ya dakika 27 ya kiungo, Jean Charles Ahoua Novemba 27, mwaka jana.
Licha ya makosa ya bao la utanguzi lililosababishwa na beki, Che Malone Fondoh, ila Simba ilicheza kwa nidhamu ya juu na kushuhudia ikiutawala mchezo katika dakika 45 za kwanza, huku wapinzani wao wakitengeneza mashambulizi kwa kushtukiza.
Katika kipindi cha kwanza timu zote zilitengeneza mashambulizi ya hatari manne ambapo nyota wa Bravos, Samuel Bengue alikosa bao la wazi dakika ya 32 ya mchezo huo, baada ya kupiga mpira kichwa akiwa peke yake na kwenda nje la lango.
Hata hivyo, baada ya kosakosa hizo, Simba ilijibu mapigo kufuatia nyota wa kikosi hicho, Kibu Denis kuupiga mpira kichwa uliokuwa unaelekea langoni dakika ya 38 na kushuhudia kipa wa Bravos, Okiemute Odah kuokoa na kuweka hai matumaini kwao.
Kibu Denis angeweza kuweka hai matumaini ya Simba ya kuchomoa bao baada ya kupiga tena mpira kwa kichwa dakika ya 41 na kugonga mwamba, kisha wenyeji kujibu mapigo dakika ya 45, kufuatia shuti kali la Joaquim Paciencia kuokolewa na Moussa Camara.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids aliamua kujilipua kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko ya mapema tu kwa kuwatoa, Yusuph Kagoma na Elie Mpanzu huku wakiingia Debora Fernandes Mavambo na Ladack Chasambi ambao waliongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
Mabadiliko hayo yalionekana ya kiufundi zaidi kwa Simba ambayo yalilenga kutengeneza mashambulizi baada ya wapinzani wao kuonekana kucheza kwa tahadhari, licha ya kuamka mwishoni mwa mchezo kwa kuliandama lango la ‘Wekundu hao wa Msimbazi’.
Sare ya Simba imeifanya timu hiyo kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikishop Afrika kwa mara ya sita kati ya saba tangu mwaka 2018, baada ya kufikisha jumla ya pointi 10, katika kundi ‘A, nyuma ya CS Constantine ya Algeria yenye 12.
Constatine imefikisha pointi hizo baada ya kuichapa CS Sfaxien ya Tunisia mabao 3-0, ambao mchezo wa mwisho wa raundi ya sita itakuwa ugenini jijini Dar es Salaam kukamilisha ratiba dhidi ya Simba Januari 19, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.