Mpepo suala la muda tu Singida Black Stars

BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi sita, taarifa zimefichua kuwa mshambuliaji, Eliuter Mpepo amemalizana na Singida Black Stars hivyo ni suala la muda tu kuanza kuitumikia timu hiyo akiwa mchezaji huru.

Mpepo alikuwa nje ya uwanja baada ya kumalizana na timu yake ya zamani Trident ya Zambia na kutua nchini akifanya mazoezi binafsi bila ya kujiunga na timu yoyote kwa miezi sita.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kuwa mshambuliaji huyo tayari amesaini mkataba na jana Jumatatu alijiunga na kambi ya timu hiyo iliyopo jijini Arusha.

“Ni kweli ameungana na timu mara baada ya kusaini mkataba, anakuwa mchezaji watatu baada ya kutambulishwa wawili kabla yake na wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa kuelekea kumalizia msimu,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.

“Uongozi bado unaendelea na mchakato wa usajili kwani hadi sasa ni wachezaji zaidi ya 15 wametolewa kwa mkopo kwenda timu mbalimbali, kuna ambao walitolewa mwanzo wa msimu wanaendelea kusalia huko lakini pia kuna ambao wamerudi na kutolewa tena.”

Mwanaspoti lilipomtafuta ofisa habari wa timu hiyo, Hussein Masanza alisema taarifa ambayo sio rasmi hawezi kuizungumzia na kama mchakato wa kumsajili juu ya mchezaji huyo upo basi taarifa itatolewa.

“Timu yetu inafanya mambo kwa uwazi sana, kila tunachokifanya huwa tunakitolea taarifa, hivyo kama suala hilo lipo mtapata taarifa rasmi. Kwa sasa timu inaendelea na maandalizi jijini Arusha,” alisema Massanza.

Wachezaji wa Singida Black Stars waliotolewa kwa mkopo hadi sasa ni Habib Kyombo, Hamad Majimengi, Mohamed Kamara wote wametua Pamba Jiji, Yahya Mbegu amepelekwa Mashujaa, Fikirin Bakari, Faria Ondongo wote Tabora United.

Wengine ni Seleman Mwalimu, Edger William wamebaki Singida Fountain Gate, Rabin Sanga, Ezekiel Mwashilindi wote wamepelekwa Tanzania Prisons.

Related Posts