Msengi aibukia JKT Tanzania | Mwanaspoti

MAAFANDE wa JKT Tanzania wanaendelea kusajili kimyakimya baada ya kuelezwa tayari wamemalizana na kiungo Ally Msengi waliyempa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Tanzania Prisons.

Taarifa za ndani kutoka JKT TZ, zinasema wamemalizana na kiungo huyo wanayeamini atakuwa msaada kutokana na uwezo alioonyesha akiwa na Prisons msimu uliopita ambako alikuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza.

“Msengi ni aina ya wachezaji ambao wana uwezo wa kumsoma mpinzani kwa haraka na akajua kipi akifanye kwa kuisaidia timu yake, hivyo tunaamini ana kitu atakiongeza akisaidiana na wachezaji waliopo,” kilisema chanzo hicho.

Msengi amewahi kuzitumikia timu kadhaa zikiwamo KMC (2018-2020), Stellenbosch (2020-2022) na Moroka Swallows (2022), jambo ambalo uongozi huo unaamini uzoefu wake utawafaa kumalizia salama duru la pili baada ya kuanza vibaya mwanzoni mwa msimu huu wakiwa maeneo la mkiani mwa ligi.

“Duru la pili ni la uamuzi timu inasalia Ligi Kuu hilo ndilo la msingi, ingawa malengo ni kumaliza katika nafasi za juu,” chanzo hicho kilisema wakati huu Prisons ikishika nafasi ya 14 kati ya timu 16 ikikusanya pointi 14 baada ya mechi 16 ikishinda 3 tu, sare 5 na kupoteza nane.

Related Posts