Mtoto afariki, wengine watatu walazwa wakidhaniwa kula sumu wakati wakicheza

Dodoma. Mtoto Jayson James mwenye umri wa miaka miwili na nusu, amefariki dunia na wenzake watatu wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kula kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu wakati wakiwa wakicheza kwenye korongo lililopo jirani na nyumba yao.

Tukio hilo lilitokea jana, Januari 12, 2025, kwenye Mtaa wa Msangalalee Magharibi, Kata ya Dodoma Makulu, Jijini Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, amethibitisha tukio hilo leo Jumatatu, Januari 13, 2025 alipozungumza na Mwananchi Digital na kusema watoto hao wanne ni kutoka familia moja.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni watoto hao kwenda kucheza kwenye korongo lililopo karibu na nyumba yao, ambapo walikuta vitu vinavyofanana na sukari au chumvi na kuanza kula.

“Hakuna mtu anayeshikiliwa kwa kosa hili, lakini bado tupo kwenye uchunguzi ili kubaini aliyehusika na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa,” amesema Katabazi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Msangalalee Magharibi, Leonard Ndama, amesema tukio hilo lilitokea saa 5 asubuhi, na kwamba baada ya watoto hao kurudi nyumbani hali zao zilianza kudhoofika.

“Bibi yao alipoona hali zao zimeharibika, aliwauliza walikula nini, ndipo walipokwenda kumwonyesha vitu walivyokula kutoka kwenye korongo, ambavyo vilikuwa vyeupe na kufanana na sukari au chumvi. Bibi yao aliwapeleka kisha haraka kwenye zahanati ya karibu, lakini mtoto mmoja alifariki kabla hajapatiwa matibabu,” amesema Ndama.

Waliolazwa hospitalini ni Jayson James (4), Yohana Chacha (5), na Caren Chacha (2), na hali zao zinaendelea vizuri.

Korongo walilokuwa wanacheza linapitisha maji yanayotumika kwenye kilimo cha umwagiliaji, na inadhaniwa kuna mtu alimwaga mbolea ya chumvi, ambayo imekuwa chanzo cha madhara hayo.

Mmoja wa majirani, Magreth Masima, amesema waliguswa na ombi la bibi wa watoto hao la msaada wa kuwapeleka hospitali, na kwamba aliona mtoto akifariki kabla ya kufikishwa hospitali.

“Baada ya kuona hivyo, uongozi wa zahanati waliwatafutia usafiri na kuwapeleka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi, huku mtoto aliyefariki akipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti,” amesema Masima.

Related Posts