Polisi TZ yambeba Kawambwa | Mwanaspoti

BAADA ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Singida Black Stars, beki Rashid Kawambwa amepelekwa Polisi Tanzania inayoshiriki Championship kuitumikia kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.

Kawambwa ni miongoni mwa wachezaji waliotolewa kwa mkopo na Singida Black Stars kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa Januari 15 mwaka huu.

“Polisi Tanzania imeonyesha nia ya kumuhitaji lengo ni kwenda kuendeleza kipaji cha mchezaji wetu huyo ambaye bado ni kijana mdogo,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.

“Kuendelea kumng’ang’ania mchezaji ambaye hana nafasi ya kucheza ni kuua kipaji chake, tunaamini kumtoa kwa mkopo ataenda kupambana na kuushawishi uongozi kumrejesha kama atafanya kitu kitakacholishawishi benchi la ufundi.”

Mwanaspoti lilimtafuta beki huyo ambaye alisema ni nafasi kwake kufanya kazi kwa kujitoa ili kuhakikisha anarudi kupambania nafasi kikosini hapo huku akiweka wazi kuwa amepelekwa sehemu sahihi kwa sababu anaenda kucheza bila presha.

“Nimepata fursa ya kutafutiwa timu naenda kupambana, naamini nina uwezo wa kufanya vizuri na nikarudi tena ligi kuu, kuhusu nafasi ushawishi wangu kwa benchi la ufundi ndio utakaonipa nafasi ya kucheza na naamini itakuwa hivyo,” alisema beki huyo.

Related Posts