Posho yaibua sintofahamu uchaguzi Bavicha

Dar es Salaam. Mkutano wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) ulisimama kwa dakika kadhaa leo, Jumatatu Januari 13, 2025, baada ya wajumbe kuhoji hatma ya posho zao za kujikimu, tofauti na ahadi walizokuwa wamepewa awali.

Tukio hilo limetokea katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya viongozi wa kitaifa kuondoka ukumbini.

Baada ya viongozi wa chama, wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu, kuondoka, mwenyekiti wa kikao aliwataka wajumbe kuanza kupitia ajenda zilizopo. Hata hivyo, mmoja wa wajumbe alisimama na kuomba ufafanuzi kuhusu posho zao za kujikimu.

“Mwenyekiti, tangu jana tumekuja hapa lakini hadi sasa hatujui hatma ya posho zetu. Je, mnataka tule kwa wagombea? Tumelala kwa shida tukitegemea mambo yangekuwa safi leo,” amehoji mjumbe huyo.

Mwenyekiti wa kikao alijaribu kutuliza hali kwa kusema suala hilo litashughulikiwa baadaye, lakini wajumbe wengi walipinga, wakisisitiza suala hilo linapaswa kushughulikiwa mara moja.

Baada ya malumbano yaliyochukua takribani dakika tano, mwenyekiti alitangaza kuwa fedha za posho ziko tayari makao makuu ya chama na zingepelekwa ukumbini. Hata hivyo, wajumbe walikataa kuendelea na kikao bila uhakika wa kupokea posho hizo.

Hatimaye, iliamuliwa wajumbe wapate chakula kwanza huku wakisubiri suluhisho la suala, jambo lililopokelewa kwa ridhaa na wote.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts