Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amewaeleza wananchi katika ziara yake ya kijiji kwa kijiji kuwa Mkoa huo unaendelea kupokea fedha kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa awamu katika kutekeleza mradi mkubwa wa maji unaogharimu Shilingi Bilioni 440 kutoka Serikali kuu.
Utakapokamilika mradi ambao utamaliza changamoto ya maji katika mkoa Mzima wa Simiyu na hivyo wananchi kuwa na uhakika wa maji safi na salama.
Mkuu wa Mkoa Kihongosi ameyasema hayo akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kijiji kwa kijiji ili kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi zinazowakabili.
Akieleza zaidi Kihongosi amesema tayari utekelezaji wa mradi huo wa maji umeanza kwa kasi kubwa na chanzo cha maji hayo kimejengwa Wilaya ya Busega na matanki mengine yanajengwa Wilaya za Bariadi na Itilima ambayo mengine yameshakamilika.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa ili azma hiyo ikamilike amewataka wananchi wa mkoa huo kudumisha amani, upendo na mshikamano kwani kama jamii italinda amani basi imelinda taifa na atakayechochea vurugu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.