Dar/Mikoani. Wakati shule za msingi na sekondari nchini zikifunguliwa kwa muitikio mkubwa, baadhi ya wazazi na walezi wameeleza changamoto za kiuchumi zinazoathiri ununuzi wa vifaa vya shule, huku kina baba wakihimizwa kushirikiana kikamilifu na watoto wao hususan wanaoanza masomo kwa mara ya kwanza.
Hali hii inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi walioandikishwa kwenye shule mbalimbali nchini kupelekwa na mama zao, huku kina wakiwa wachache.
Shule za msingi na sekondari zimeanza rasmi muhula mpya wa masomo leo Jumatatu, Januari 13, 2025, huku wanafunzi wa madarasa ya awali, la kwanza na kidato cha kwanza wakiianza safari yao ya masomo rasmi.
Yusuph Mwankemwa, mkazi wa Ilolo, Mbeya, akizungumza na Mwananchi, amesema licha ya wazazi kuonyesha muitikio wa kuwaandikisha watoto wao shule, idadi kubwa ya wanawake ndiyo wanaonekana kuwapeleka watoto shuleni, huku wanaume wakihusika kwa uchache, hali ambayo inazua wasiwasi.
Amesema ukaribu wa mtoto na mzazi mmoja tu, hususan mama, unaweza kupunguza mapenzi kwa mzazi mwingine, akishauri ushirikiano kati ya wazazi wote wawili katika masuala ya elimu ya watoto.
“Nimeshangaa wanaume tuko wachache sana hapa shule ya Kambarage, hatufiki hata wanne, ilhali wanawake ni wengi. Mtoto ni wa baba na mama, kila mmoja anapaswa kushirikiana kumlea kielimu na kisaikolojia,” amesema Mwankemwa.
Kwa upande mwingine, Khalid Juma, mkazi wa Chanika, Handeni, Tanga, ameelezea changamoto ya kupanda kwa bei ya vifaa vya shule kama sare, viatu na mabegi, hali inayowalemea baadhi ya wazazi.
“Kaptula na sketi zinauzwa kati ya Sh7,000 hadi 10,000 na hapo hujazungumzia mashati. Bei hizi si rafiki,” amesema Khalid.
Huku Khalid akilalamikia gharama za vifaa vya shule, Salome Mwawalo, mkazi wa Songwe, amepongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya madarasa, akisema uboreshaji huo umewahamasisha watoto kwenda shule. “Watoto wanavutiwa na madarasa mazuri; wengine hata wanasisitiza wenyewe kupelekwa shule,” amesema Mwawalo.
Teresia Michael, aliyekuwa Shule ya Msingi Mabibo, Dar es Salaam, amesema kuwa mchakato wa kumuandikisha mwanawe ulianza mapema ingawa haukuwa rahisi.
“Tulitakiwa kuwasilisha cheti cha kuzaliwa cha mtoto, namba ya Nida ya mzazi, na mtoto alipaswa kuonyeshwa sehemu ya kusoma ili mwalimu ajue kiwango chake cha usomaji,” amesema Teresia.
Kwa upande wake, Munira Salim, mkazi wa Dar es Salaam, ameelezea malalamiko yake kuhusu walimu kumtaka anunue vifaa vingine tofauti na maelekezo ya awali.
“Tulipewa orodha ya mahitaji, lakini leo naambiwa faili nililonunua halifai, wanataka faili jingine,” amesema kwa masikitiko.
Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, iliyopo Manispaa ya Moshi, Laurence Kisima amesema mwitikio wa wanafunzi kuripoti shule umekuwa wa kuridhisha kwa wale waliojiandikisha.
“Kwa uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza mwaka 2025, ambapo jumla ya wanafunzi 1,290 walijiandikisha, tumefikia asilimia 100, na hatujakutana na changamoto yoyote,” amesema Kisima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Mlimani, Halmashauri ya Mji Handeni, mkoani Tanga, William Kimaro, alisema shule yake inapokea watoto wote bila kujali kama wanavaa sare mpya au za zamani.
“Haturuhusu mtoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya sare au ada. Kipaumbele ni madaftari, kalamu, na mahitaji mengine ya darasani,” amesema Kimaro.
Katibu Tawala Msaidizi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi mkoani Songwe, Majuto Njanga, alisema kuwa jumla ya wanafunzi 92,986 wanatarajiwa kuanza masomo ya awali, darasa la kwanza, na kidato cha kwanza mkoani humo.
“Maandalizi yamekamilika, ikiwa ni pamoja na madarasa kwa ajili ya wanafunzi hao. Kila mzazi na mlezi awajibike kumpeleka mtoto shule, na yeyote atakayebainika kuficha mtoto atachukuliwa hatua za kisheria,” ameongeza Njanga.
Mkuu wa Shule ya Msingi Tabata, Alex Mugisha, ametoa wito kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shule mapema ili wasipitwe na masomo ya mwanzo.
“Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwahisha watoto wao shuleni mapema ili waweze kufuata masomo bila kukosa mambo muhimu ya awali,” amesema Mugisha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Amri Mkalipa ameagiza wenyeviti wa serikali za mitaa kufanya msako wa nyumba kwa nyumba kubaini watoto waliofikisha umri wa kwenda shule lakini hawajapelekwa.
“Karibuni nitaanza ziara ya kijiji kwa kijiji na mtaa kwa mtaa kusikiliza na kutatua kero za wananchi. Sitaki kusikia kuwa kuna watoto wanaostahili kuwa shule lakini hawajaenda. Hakikisheni kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapelekwa bila visingizio,” amesema Mkalipa.
Imeandikwa na Saddam Sadick (Mbeya), Rajabu Athuman (Tanga), Mariam Mbwana na Mintanga Hunda (Dar es Salaam), Denis Sonkonde (Songwe), Bertha Ismail (Arusha) na Janeth Joseph (Moshi).