LIGI Kuu Bara imesimama huku ikiwa zimeshachezwa jumla ya mechi 124 zilizokusanya mabao 265 yakiwamo 110 yaliyofungwa na nyota wa kigeni 47 na mengine 148 yaliyowekwa wavuni na wazawa 80 mbali na saba ya kujifunga, lakini vigogo Simba na Yanga wakiwa hawachekani kabisa katika msimamo.
Ndio, licha ya Simba kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Yanga, vigogo hao wamegawa idadi ya mechi walizoshinda nyumbani na ugenini, wakiizidi Azam FC iliyopo nafasi ya tatu katika msimamo huo wa ligi inayotarajiwa kurejea tena Machi Mosi mwaka huu.
Ipo hivi. Yanga inayopambana kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo inabebwa na uwiano wa mabao ya kufunga ikiongoza orodha ya klabu zilizoshinda mechi za ugenini, wakati watani wao Simba wenyewe wakionekana ni wakali zaidi wanapokuwa uwanja wa nyumbani.
Katika mechi saba ilizocheza ugenini, Yanga imeshinda zote na kufunga mabao 12 bila kuruhusu wavu wa timu hiyo kuguswa hata moja, tofauti na Simba ambayo licha ya kucheza na kushinda idadi sawa na vijana wa Jangwani, imekubali kufungwa mabao mawili huku yenyewe ikifunga pia 12.
Azam ndio inayoshika nafasi ya tatu katika orodha hiyo kwa mechi za ugenini ikicheza nane na kushinda michezo mitano, ikitoka sare mbili na kupoteza mmoja, japo nayo imefunga mabao 12, ila imefungwa matatu, ilihali timu dhaifu kwa ugenini ikiwa ni KenGold iliyocheza mechi tisa na kupoteza zote.
Wageni hao wa Ligi Kuu wamefungwa mabao 18 na kufunga matatu, hawajavuna pointi hata moja ugenini, wakizidiwa na Kagera Sugar ambayo katika mechi saba za ugenini imeambulia sare mbili na kufungwa saba.
Kwa timu zilizofanya vyema nyumbani, Simba imefunika kwa kuizidi Azam inayolingana nayo idadi ya mechi ilizocheza, kushinda, kutoka sare na kupoteza ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba imefunga mabao 19 na kufungwa matatu katika mechi hizo nane za nyumbani ikishinda sita na kutoka sare moja na kupoteza moja kama ilivyo kwa Azam, lakini Wanalambalamba wamefunga mabao 13 tu na kufungwa matano, wakiwa juu ya Yanga iliyocheza pia michezo minane, lakini ikiwa haina sare yoyote ikishinda pia sita na kupoteza mara mbili.
Hata hivyo, Yanga imeonekana ndio timu iliyofunga mabao mengi nyumbani ikitupia 20, japo imefungwa sita na kukusanya jumla ya pointi 18, moja pungufu ya ilizovuna Simba na Azam, huku KenGold ikiwa pia ndio timu dhaifu zaidi kwa mechi za nyumbani ikicheza mechi saba na kushinda moja tu, ikipoteza tatu sawa na idadi ya sare, hivyo kuvuna pointi sita tu ambazo ndizo ilizoiweka mkiani mwa msimamo wa ligi.
Timu inayofuata baada ya KenGold kati ya zilizofanya vibaya nyumbani ni Namungo ikicheza pia mechi saba, ila imeshinda mbili na kutoka sare moja na kupoteza nne, ikivuna pointi saba kama ilizonazo Pamba Jiji iliyopo juu yao iliyoshinda mechi moja kati ya saba ilizocheza ikitoka sare nne na kupoteza mbili tu.
Pamoja na vigogo kushindwa kuchekana katika idadi ya pointi ilizovuna katika mechi 15 ilizocheza za duru la kwanza, lakini hata nyota wa vikosi hivyo, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala kwa Simba na Clement Mzize, Prince Dube na Pacome Zouzoua nao hawachekani vilevile katika orodha ya wafungaji.
Nyota hao wote wapo nyuma ya kinara wa mabao Elvis Rupia wa Singida BS mwenye mabao manane anayongoza hadi ligi iliposimama Desemba 29, mwaka jana.
Ahoua anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji akiwa na mabao saba, wakati Mzize ni wa tatu akiwa na mabao sita kama aliyonayo Seleman Mwalimu wa Fountain Gate aliyeongoza orodha hiyo kwa muda mrefu kabla ya kuja kupitwa na Mkenya huyo wa Singida.
Dube na Pacome wenyewe wanafuata wakiwa na mabao matano kila mmoja, wakati Mukwala amefunga mabao manne kama aliyonayo beki wa Yanga, Ibrahim Bacca na wakali wa timu nyingine katika orodha hiyo.
Hata hivyo, Ahoua na Pacome wanalingana kwa wachezaji walioasisti wakishika nafasi ya pili sambamba na Salum Kihimbwa wa Fountain Gate kila mmoja akiwa nazo tano, nyuma ya kinara Feisal Salum ‘Fi Toto’ wa Azam mwenye asisti tisa hadi ligi iliposimama.
Nyota wengine wa Simba na Yanga wanaofuata katika orodha ya wakali wa kuasisti ni, Stephane Aziz KI akiwa na nne, huku Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Ladack Chasambi wote wa Simba na Mzize wanafuata kila mmoja akiwa na tatu wakichuana na wakali wa timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo.
Hii ikiwa na maana wakati Ligi ikirudi kumalizia mechi 116 za kukamilisha msimu wa 2024-2025 ni wazi kutakuwa na vita kubwa baina ya vigogo hivyo ambapo sasa zitakuwa na mechi saba za nyumbani na nane za ugenini, mbali na mchuano wa nyota wa klabu hizo kuwania rekodi mbalimbali kwa msimu huu.
Msimu uliopita Yanga ilifanya kweli kwa kubeba ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, pia ikitoa mfungaji bora, Aziz KI aliyefunga mabao 21 akimpiku Fei Toto wa Azam aliyefunga 19, lakini kiungo mshambuliaji huyo wa Jangwani akimaliza na asisti nane nyuma ya kinara Kipre JR aliyekuwa Azam aliyekuwa na tisa.