TLS yataka wadau kusaka mwafaka wa kitaifa

Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimetaka wadau wa kisiasa, viongozi wa dini, taasisi za umma na wataalamu kukutana pamoja kujadiliana masuala yanayoitatiza nchi ili kuufanya mwaka 2025 kuwa wa mwafaka wa kitaifa.

Chama hicho kimeangazia mambo manne yanayopaswa kujadiliwa ili kupata mwafaka wa kitaifa kuwa pamoja na kuheshimiwa kwa misingi ya utawala bora na demokrasia, matukio ya watu kupotea, kufuatwa kwa utawala wa sheria na Tanzania kurejea kwenye kipengele Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu (AfCHPR).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 13 jijini Dar es Salaam na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amesema mwafaka ni muhimu nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu.

“Mwafaka wa kitaifa ni mkubwa na una hadhi kuliko hata mabadiliko ya katiba. Tuazimie wote kwamba tunataka Taifa liweje, tunataka tufanyeje, kuna mazingira ambayo tunapokwenda kwenye uchaguzi, hili Taifa lazima tusikilizane,” amesema.

Kuhusu utawala bora na demokrasia, Mwabukusi amesema kuna haja ya kuwa na mjadala kuhusu uwazi, uwajibikaji, kuheshimu mawazo tofauti na kujenga taasisi imara zinazotanguliza maslahi ya umma.

Ameeleza haja ya kuwa na taasisi imara za kusimamia demokrasia, akiitaja Ofisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya siasa yenye wajibu wa kulea vyama hivyo.

“Tunashauri ofisi hiyo kuongezewa uwezo wa kusimamia majukumu yake ili kuepuka kazi zake kufanyw ana polisi.

“Endapo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ingefanya wajibu wake, tusingeona bunduki, mabomu au askari wengi kwenye usimamizi wa shughuli za kidemokrasia,” amesema.

Ameitaja pia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi akitaka pia ijifunze kwa mambo yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 2024 uliozua malalamiko kwa vyama vya upinzani, huku akilitaka pia Jeshi la Polisi kuonyesha weledi.

Kwa upande Mwingine, Mwabukusi amewataka viongozi wa siasa kuzingatia misingi ya sheria na kuepuka kuwagawa wananchi, bali wajenge umoja wa kitaifa.

“Tumeshuhudia changamoto zinazohusiana na kauli na vitendo vyenye muelekeo wa kibaguzi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa, hii inapaswa kukomeshwa mara moja,” amesema Mwabukusi.

“Tuna uhuru wa maoni, lakini uhuru huu usivuke mipaka ya kuingilia faragha utu, hadhi na dini za watu,” amesema.

Kuhusu matukio ya utekaji, kiongozi huyo amesema vinahitaji mjadala wa kina kwani vinalitia doa Taifa.

“Vitendo hivi vinakwenda kinyume kabisa na misingi ya utu, haki na uhuru wa binadamu, hivyo tunashauri kuridhiwa kwa mkataba huo  wa watu waliopotea ikiwemo kuundwa kwa Tume ya kitaifa itakayoshughulikia mambo hayo na iwe na watu wenye ueledi watakaoaminika kwa jamii pale itakapofanya maamuzi,” amesema Mwabukusi.

Mwabukusi pia ameitaka Serikali kurejea kwenye kipengele cha Mahakama ya ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kinachoruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuishtaki Serikali baada ya kupita mwaka mmoja tangu ilipoandika kusudio la kujiondoa.

Tanzania iliandika kusudio la kujitoa kwenye kifungu cha 34(6) cha Mahakama hiyo Novemba 21, 2020.

“Ni aibu mahakama hiyo ipo nchini kwetu lakini sisi hatupo, kwani ukiacha mbali na masuala ya haki lakini pia itachohea uchumi wetu,” amesema Mwabukusi.

Akijadili suala hilo, mchambuzi wa msuala ya siasa na jamii, Faraja Kristomus ameunga mkono akisema licha ya kuwepo kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, bado imekuwa ikikuukwa.

“Kuwepo kwa mkutano huo wa mwafaka ni muhimu, kwani utasaidia kupatikana kwa Tume huru ya uchaguzi.

“Kuwepo kwa malalamiko yote haya ni kutokana na kutokuwepo utashi wa viongozi wetu kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki.

“Pia pamoja na kuwepo kwa sheria mpya za uchaguzi, tunaona bado haijasaidia, tukirejea yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema.

Related Posts