Dar es Salaam. Patachimbika ndilo neno linaloakisi uhalisia wa joto linaloendelea kufukuta katika uchaguzi wa viongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya miamba miwili Freeman Mbowe na Tundu Lissu wanaowania uenyekiti wa chama hicho.
Nguvu zao kisiasa ndani na nje ya Chadema zimeendelea kujidhihirisha katika uchaguzi wa mabaraza ya vijana (Bavicha) na wazee (Bazecha) uliofanyika kuanzia leo Jumatatu asubuhi Januari 13, 2025 maeneo mawili tofauti na kufikia tamati usiku.
Mkutano mkuu wa Bazecha umefanyikia makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam huku wa Bavicha ukifanyikia ukumbi wa Ubungo Plaza.
Kote huko kumeshuhudiwa nguvu na umaarufu wa makundi mawili yanayowaunga mkono Mbowe na Lissu.
Mbowe anayetetea nafasi hiyo ya uenyekiti aliyoiongoza kwa miaka 21, anachuana na makamu wake-bara, Lissu kwenye uchaguzi utakaofanyika Januari 21, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Joto la uchaguzi wa Bavicha na Bazecha linatokana na mchuano wa wagombea wa mabaraza hayo, jinsi wajumbe wa mikutano mikuu hiyo wanavyozifungamanisha chaguzi hizo na uchaguzi wa viongozi wa juu hususan nafasi ya uenyekiti.
Kambi hizo, zilishuhudiwa zikijipambanua kupitia matukio ya ufunguzi wa mikutano hiyo.
Imeanza kwa Mbowe na Lissu kufungua mkutano wa Bazecha kisha wawili hao kwa pamoja wakaenda kufungua ule wa Bavicha ambako huko ndiko hali ya makundi ya wawili hao ilipodhihirika.
Jinsi Lissu na Mbowe walivyopokewa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Bavicha, kumeibua mijadala maeneo mbalimbali hususan mitandaoni kwa vipande vya video kuunganishwa vikiwaonesha walivyopokewa.
Katika mikutano yote mwili, Mbowe na Lissu walizungumza na wajumbe wa mikutano hiyo.
Lissu alisimama kusalimia huku Mbowe akiifungua kwa nafasi yake ya uenyekiti. Pamoja na mambo mengine, wawili hao walitoa nasaha kuhakikisha wanachagua viongozi watakaokwenda kukijenga chama hicho.
Katikati ya minyukano inayoashiria kugawanyika, chama hicho kinachotumia kauli mbiu ya ‘Stronger Together,’ kwenye matukio ya hivi karibuni ya vikao vya kamati kuu, kamati tendaji ya Bavicha, mkutano mkuu wa Bavicha wanachama wamekuwa wakishikana mikono kuashiria umoja.
Akiufungua mkutano mkuu wa Bazecha, Mbowe amesema chama hicho kimepitia changamoto kubwa, akibainisha mnyukano unaoendelea kwa sasa katika kusaka nafasi za uongozi.
“Wote ni mashahidi, kwa miaka saba chama hiki kilijaribiwa kwa kila aina. Tulitupiwa mashetani ya kila aina, na haikuwa kwetu pekee bali hata kwa vyama vingine vya upinzani. Lakini kwetu tulibaki kuwa mashujaa.
“Majaribu yalikuwa mengi, kwa wabunge, madiwani na kuna waliopoteza uhai kwa ajili ya kukipigania chama hiki.
“Nawataka wazee muendelee na ustahimilivu na kujivunia kwa kuwa, mlisimama imara kukipigania. Wanaotaka kutufarakanisha na mashetani yao, tuwakatae, kwani itakuwa laana, na kukiua chama hiki itakuwa uhaini,” amesema Mbowe.
Amesema safari ya Bazecha haijawahi kuwa rahisi, kwa kuwa walikumbana na milima na mabonde, wakiumwa na ng’e lakini walivumilia na hatimaye kufika hapo.
Mbowe amesema kukiangamiza chama hicho ni uhaini kwa kuwa, kimebeba maono ya Watanzania wanaopambana na changamoto mbalimbali.
“Wakati nakabidhiwa uongozi wa chama hiki miaka 21 iliyopita, hakukuwa na Baraza la Wazee, itifaki wala kanuni. Hivyo ni wajibu kwa kila mmoja anayeona ana maoni, milango iko wazi,” amesema.
“Chama hiki si cha Mbowe pekee. Chama hiki si Biblia. Nyaraka za chama hiki zinafanyiwa rejea na kubadilishwa. Tuache kutengeneza fitina,” amesema Mbowe.
Katika mkutano mkuu wa Bavicha, Mbowe amewaonya vikali dhidi ya tabia za mivutano na maneno yasiyofaa yaliyodhihirika katika mchakato wa uchaguzi wa chama mwaka huu, akisisitiza si sehemu ya utamaduni wa Chadema.
“Kwa tabia iliyoonyeshwa mwaka huu, si utamaduni wa Chadema. Tunahitajiana wote ili kutimiza mahitaji ya Chadema. Pepo lolote lenye dhana ya kututenganisha hatupaswi kulilea; lishindwe kwa nguvu zote.”
Mbowe amekiri kuna changamoto za kawaida katika mchakato wa uchaguzi, lakini amesisitiza umuhimu wa mshikamano baada ya uchaguzi kukamilika.
“Ni kweli tutanyukana, lakini tukimaliza kunyukana tutakutana kwenye boksi. Tukishamaliza kwenye boksi tushikane mikono, tuone tunaendaje,” amesema.
Awali, katika mkutano wa Bazecha, Lissu amesema:“Naomba niwashukuru waliotumikia nafasi hii kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Lakini naamini leo tutapata safu mpya ya kujenga matofali. Wakati huu, baada ya leo nitakuwa na miaka 58. Wazee wenzangu, heri ya mwaka mpya kwa wale ambao hatujakutana.”
“Naomba nisiwapotezee muda. Niwatakie kila la heri. Tuchague viongozi kwa uchaguzi ulio huru na wazi kama inavyosema Katiba yetu ili waongoze kwa miaka mitano ijayo,” amesema Lissu.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Bavicha, Lissu, ametoa wito kwa vijana kuhakikisha wanachagua viongozi wanaotambua wajibu wao kwa Taifa, si kwa vijana pekee bali kwa masilahi mapana ya nchi.
Lissu amesema: “Vijana wa kila rika wana jukumu la kutambua wajibu wao kwa nchi yao. Wanaoelewa wajibu wao hufanya mambo makubwa, uchaguzi wa viongozi wa Bavicha ni fursa ya kupata viongozi wanaotambua wajibu wa vijana kwa Taifa,” amesema Lissu.
Amesema ni vijana pekee wenye uwezo wa kuwa jasiri na kupigania mabadiliko katika kila zama na nchi.
Moja ya hotuba katika mkutano wa Bavicha iliyokonga nyoyo za wajumbe ni ya Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu ambaye mara kadhaa walikwenda kumtunza fedha kutokana na kile alichokuwa akikizungumza hususan akikemea rushwa.
Pambaluamewahimiza viongozi watakaochaguliwa kupigania haki, kuweka mbele ajenda za vijana na kujiepusha na siasa za rushwa. Amewataka viongozi wapya kuhakikisha wanajenga mshikamano wa kweli na kuwa sauti ya vijana wanaokandamizwa na mfumo wa kidhalimu.
“Jengeni umoja, ustahimilivu na mshikamano huku mkipaza sauti kwa wenzetu waliotekwa na wenzetu wenye roho mbaya katikati ya mapambano. Mkiwachagua viongozi kwa sababu waliwalaza na kuwapa Sh20,000 …laana itakuwa juu yenu,” amesema Pambalu huku akishangiliwa.
Amesisitiza viongozi wa Bavicha wanapaswa kuwa mfano wa uwajibikaji na kujituma, huku akionyesha dhamira yake ya kuendelea kupigania ukombozi hata baada ya kumaliza muda wake.
“Nagombea nafasi ya mjumbe wa Kamati Kuu, lakini hata nikishindwa, nitaendelea kuhubiri ukombozi vijiweni,”amesema.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto amewaambia wajumbe wahakikishe wanachagua kiongozi sio kwa kuangalia anamuunga nani mkono.
Badala yake, amewataka wachague viongozi wanaostahili kuliongoza baraza hilo.
Amesisitiza wachague kiongozi atakayekipambania chama na sio kuangalia nani anayemuunga mkono katika uchaguzi wa kitaifa.
“Msikubali mtu yeyote katika chama hiki, baada ya uchaguzi akakuletea maneno kwamba, hakukuwa na haki hakukuwa na nini, uchaguzi ukiisha tunafanya kazi pamoja,” amesema.
Heche: Vijana msiwe sehemu ya ufisadi
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa baraza hilo amewataka vijana kutambua nafasi yao muhimu katika kuleta mabadiliko na kuhakikisha uongozi bora unapatikana bila kuwa sehemu ya ufisadi.
“Vijana wa nchi hii iliyojaaliwa rasilimali za kila aina, tuna ziwa pana kuliko yote duniani, tuna madini ya nikeli, tuna dhahabu kila kona, tuna ardhi, tupo kwenye nchi tajiri lakini watu wake ni maskini,” amesema Heche.
Amewaasa vijana kutokuwa sehemu ya ufisadi wa kisiasa kwa kuepuka kuwachagua viongozi watoa rushwa.
“Kama kuna mtu amekupa Sh100, usimpe kura yako kwa sababu tuna historia katika baraza hili.”
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama amewataka wajumbe hao kutumia demokrasia kwa tija kuchagua viongozi wenye maono.
“Tambueni mkifanya vibaya jahazi hili likijaa itachukua muda kurudisha uhai wake, demokrasia tunayozungumzia imeasisiwa na nchi za magharibi zinaruhusu kwa kuweka mifumo ya kuchaguana kupata viongozi wa kuwakilisha wengi, hivyo mtakaochukua kijiti tambueni mnayo majukumu mengi,” amesema.
Katika mkutano huo, mvutano uliibuka kati ya wasimamizi wa uchaguzi wa Bavicha na wajumbe, wakigomea kufanya uchaguzi hadi watakapolipwa posho zao za siku tatu na nauli za safari kutoka mikoa mbalimbali.
Mvutano huo ulianza muda mchache wakati zinatangazwa itifaki za kuelekea kufanyika kwa uchaguzi, wajumbe walitaka walipwe kwanza posho hizo kabla ya lolote kuendelea.
Baada ya kuibuka hoja hiyo, viongozi waliwataka waende kula kwanza kisha kabla hawajaingia kuendelea na mkutano wa uchaguzi watalipwa ndio uchaguzi uendelee.
Wajumbe walikwenda kula kisha kurudi ukumbini, lakini hakukuwa na fedha walizoahidiwa wangepewa.
Hali hiyo, ilisababisha wajumbe waendelee kugomea mkutano huo na ndipo msimamizi wa uchaguzi huo, Salum Mwalimu alipowapa machaguo matatu.
Chaguo la kwanza, Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu- Zanzibar amesema ni ama watoke nje hadi watakapolipwa posho zao ndio waingie ndani na aliwataka watu wanyooshe mkono.
Hakuna mjumbe aliyenyoosha mkono baada ya kuulizwa hilo.
Chaguo la pili, Mwalimu amesema uchaguzi uendelee kisha watalipwa baadaye, wajumbe wote walipinga hilo.
Chaguo lingine, amesema uchaguzi ufanyike kabla haujaisha fedha ziwe zimefika na usimamishwe ili walipwe kwanza.
Katika chaguo hilo, kulikuwa na majibu mawili wapo waliounga mkono na wengine walipinga hilo na hivyo kuibuka mizozo.
Hadi muda huo, ilishapita nusu saa kabla ya mchakato wa uchaguzi kuendelea wajumbe walikuwa wakaendelea kuvutana na Mwalimu.
Hatimaye, Mwalimu aliwataka wajumbe wenye chaguo mbadala na hayo waende nje wakajadili kisha waje na pendekezo lao.
Mmoja wa wajumbe aliyekwenda mbele, amesema kauli ya kuambiwa watoke nje kujadili hoja mbadala inawaogopesha wajumbe.
Dakika chache baada ya mvutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliingia na kueleza wameandaa mkutano huo kila mmoja atalipwa fedha zake.
“Hakuna mtu atakaye kula kwa fedha zake binafsi wala atakayekuja kwa fedha zake binafsi,” amesema.
Amesisitiza hakuna fedha itakayopotea na kilichochelewesha ni taratibu za fedha, ambao lazima malipo yafanyike kwa risiti.
“Chama kikimtumia kijana nyumbani fedha na asitokee kwenye mkutano, ikikosekana tiketi CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) akija kukagua inaonekana kama Makao Makuu mmeshirikiana na watu fulani kutafuna fedha,” amesema.
Amesema wameweka utaratibu wa kuhakikisha kila anayefika ndiye anayepewa fedha ya kujikimu na atatoa tiketi ya safari yake kisha kulipwa nauli ya kwenda na kurudi.
Amewataka wawe wavumilivu huku akisisitiza haki za pande zote zizingatiwe.
Kamati ya Uchaguzi yateuliwa
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ametangaza Kamati ya Wazee Wastaafu wa chama hicho watakaosimamia uchaguzi wa chama hicho ngazi ya Taifa.
Mnyika amesema uteuzi wa wazee wastaafu umefanywa na Kamati Kuu katika kikao chake cha Januari 11, 2025.
Walioteuliwa ni, Ahmed Rashid, Alfred Kinyondo, Profesa Azaveli Lwaitama, Wakili Edson Mbogoro, Francis Mushi, Lumuli Kasyupa, Profesa Raymond Mosha na Ruth Mollel aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Utumishi.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Bakari Kiango, Baraka Loshilaa na Tuzo Mapunda