Dar es Salaam. Utawala bora wa sheria, elimu, afya, uchumi na familia ni miongoni mwa vinavyopaswa kufanyiwa kazi zaidi katika uandaaji wa dira ya Taifa 2050, imeelezwa.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Januari 13, 2025, katika mkutano wa Kamati za Dini Mbalimbali wa kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uliofanyika kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Kurasini jijini hapa Dar es Salaam.
Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa amesema kama nchi inatengenezwa dira ambayo haiweki vizuri uhuru wa watu ni sawa na kujitekenya na kucheka mwenyewe.
Amesema kama nchi inataka kuwa na watu wanaojiamini, ni vyema dira iweke wazi kuwa, lazima wajengewe uwezo wa kujiamini na kusema mambo yao kwa uhuru.
“Huwezi kuwa na mawazo tofauti…. basi unaanza kuulizwa hata uraia wako we mtu wa wapi, haya matatizo yapo hasa kwenye miji ya mipakani, ukipingana tu na wakubwa unaulizwa wewe asili yako wapi, wewe Mrundi, wewe siyo Mkongomani,” amesema Kiburwa.
Amesema si vyema kumtisha mtu kwa sababu amezaliwa Kigoma, Bukoba au Ngara kwa kutaka kuangalia uhalali wa uraia wake huku akitaka dira iwajengee watu uwezo wa kujiamini kwa kuonyesha watu wanatakiwa kuishi katika nchi ambayo hawatishwi.
“Unaweza kusema mawazo yako na yakakubalika, ukishajenga watu ambao hawatishwi utapata michango mizuri kutoka kwa watu watakaotoa maoni wanayoyaamini katika mioyo yao, zaidi ya hivyo tutakuwa tunajenga Taifa la watu wanafiki, wanaopenda kujikomba, kujipendekeza baadaye inakuwa ni maafa kwetu,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Sheikh Mohamed Khamis ameitaka tume ifanye tathmini na kuzingatia changamoto zilizojitokeza katika dira ya mwaka 2025 na kuangalia namna ya kukabiliana nazo katika utekelezaji dira ya 2050.
Miongoni mwa changamoto alizoainisha ni kutofungamana moja kwa moja kwa sera mbalimbali ikiwamo ya vyama vya siasa na dira ya mwaka 2025.
“Matokeo yake ilikuwa ni kukosekana kwa vipaumbele vya kudumu vya Taifa katika shughuli za vyama vya siasa,” amesema Sheikh Khamis.
Pia, ameitaka dira ya mwaka 2050 kuimarisha mazingira ya amani, usalama na umoja kwa vitendo kwa kuzingatia falsafa ya maridhiano yaani ustahamilivu, mageuzi na kujenga upya.
“Pia, uhuishaji wa mchakato wa Katiba uzingatie mahitaji ya sasa na masilahi mapana ya Taifa, pia iweke mkazo wa sera za kudumu za Taifa hata kama Serikali itabadilika kupitia mzunguko wa uchaguzi,” amesema.
Katika kuboresha amani, utulivu na utawala bora, Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Azgard Stephen amesema matatizo makuu ya mwanadamu ni umaskini, ujinga na maradhi; endapo vikishughulikiwa hali itakuwa shwari.
Amesema mtu mwenye njaa, mjinga na mwenye magonjwa, hawezi kuchagiza amani hivyo ni vyema afya, ustawi wa jamii na elimu bora ingekuwa ni msingi wa dira katika kipindi hiki.
“Mwaka jana tumehuisha mtalaa wetu wa elimu na kuweka ule wa amali sasa, ili kuweza kuutekeleza mtalaa huu kwa kupata matokeo, basi tungeweka elimu na afya katika msingi imara, kwa kuwa tumetandaza mtandao wa vituo vya afya na zahanati nchini lakini uwezo wake si mkubwa,” amesema Stephen.
Katika uchumi, Stephen amesema ili kufikia biashara ya kimataifa, diplomasia ya Tanzania na nchi nyingine inapaswa kuwa kichocheo kikubwa kufikia biashara ya kikanda na kimataifa.
“Dira ingeonyesha urahisi wa sheria katika kufanya biashara, kuna mlolongo mkubwa wa vibali, ni vyema kuweka urahisi ili watu wanapofanya biashara ya kikanda iwe rahisi, tunajua zipo juhudi nyingi zinazofanyika kupunguza mlolongo huu ikiwamo kuhamasisha matumizi ya kidijitali, lakini tumeona ikiwa kwenye sera inakuwa rahisi zaidi,” amesema Stephen.
Katika mazingira ya biashara, amesema kodi kubwa imekuwa ikilalamikiwa na kusababisha baadhi ya wafanyabiashara waikwepe, huku akipendekeza dira iweke maono ya kupanua wigo wa kodi kwa kuweka mfumo wa ulipaji kodi himilivu kwa wafanyabiashara.
“Dira inaonyesha kuwa, mashirika ya umma yana mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo huku yakitaka sekta binafsi ipewe msukumo zaidi ili Serikali isibebe mzigo wa kufanya biashara badala yake iweke mazingira wezeshi katika uchumi ili wananchi washiriki huko,” amesema Stephen.
Kuhusu familia, afya na elimu
Sheikh Khamis amependekeza kuwapo kwa taarifa za kiuchumi na takwimu kuanzia ngazi ya familia ili kuboresha uamuzi na kudhibiti kamari ambayo imekuwa ikiwatia vijana ufukara na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Katika afya, ametaka hospitali na vituo vya afya kujengwa hadi ngazi ya vijiji na kupunguza gharama za matibabu na kuhamasisha utalii wa ndani kwa kupunguza gharama.
Hili likiwekewa mkazo zaidi katika kufanikisha bima ya afya kwa wote kwa kutenga sekta moja ya kiuchumi, ambayo ndiyo itakuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kugharamia matibabu.
Katika elimu, Sheikh Khamis amesema ni vyema sera na miongozo zikasomana.
“Mfano baada ya kuanzisha mafunzo ya amali, mwanafunzi anapomaliza kidato cha nne akiwa na cheti cha elimu ya amali, je umri wake utaruhusu kuajiriwa kuendana na Sheria ya Ajira,” amehoji.
Pia, ameitaka elimu inayotolewa itambulike duniani ikiwamo ile ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), fedha na biashara kuanzia ngazi ya awali huku ujumuishi wa utoaji elimu uimarishwe hususan katika maeneo yaliyoachwa nyuma kulingana na historia, mila au nyinginezo.
“ Pia, tuboreshe masilahi ya walimu ili kuvutia walimu waliofaulu vizuri kujiunga na fani ya ualimu,”amesema Sheikh Khamis.
Msemaji wa TEC, Dk Camilius Kasala amesisitiza umuhimu wa kuzingatia familia na vijana kama nguzo kuu za maendeleo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dk Kasala amesema vijana ni kundi muhimu linalohitaji kupewa elimu, ujuzi na nyenzo za kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo.
“Vijana wanapaswa kupewa mazingira, nyenzo, stadi, elimu na ujuzi wa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo hadi mwaka 2050. Ni muhimu kuhakikisha wanapata ajira za kipato cha uhakika kupitia vyama vya ushirika, vikundi vya kiuchumi na shughuli zinazozingatia jiografia na hali ya hewa ya maeneo yao,” amesema Dk Kasala.