Wajumbe Bazecha waanza kupiga kura, wagombea walivyojinadi

Dar es Salaam. Wajumbe wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) wameanza kupiga kura kuwachagua viongozi mbalimbali watakaoongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mkutano Mkuu wa uchaguzi unafanyika leo, Jumatatu, Januari 13, 2025, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Kabla ya wajumbe kuanza kupiga kura, saa 1:27 usiku, kamati inayosimamia uchaguzi huo, ikiongozwa na Alfred Kinyondo, ilianza kufanya uhakiki wa karatasi za kupigia kura kwa kuzihesabu na kuwataja wagombea kulingana na namba zao.

Muda uliotumika kuhakiki majina na namba za wagombea ulikuwa wa kutosha, na uliwapa wagombea nafasi nyingine ya kuzunguka kwa wajumbe kuomba kuaminiwa ili wapate fursa ya kuongoza baraza hilo.

Maombi ya wagombea kwa wajumbe yalisababisha minong’ono ukumbini humo, huku meza kuu ikiendelea kuwa na utulivu, nyuso za wajumbe zikiashiria umakini mkubwa wakati wa kuhakiki majina ya wagombea.

Kuanzia saa 12:15 jioni, ilipotangazwa kukamilika kwa fursa ya wagombea kujinadi na kuomba kura, hadi saa 1:00 usiku, sauti za wagombea na wajumbe zilikuwa zikitawala ukumbi, huku muziki wa hamasa “Chadema! Chadema! People’s Power!” ukiendelea kuchangamsha hali.

Hakukuwa na dosari yoyote hadi uchaguzi ulipoanza rasmi, kwani akidi ya wajumbe walioshiriki ilikuwa asilimia 81 kutoka mikoa yote 34 ya chama hicho nchini, kiwango kilichozidi lengo la kikatiba la asilimia 75 ya wajumbe wanaohitajika kupiga kura.

Wagombea wa nafasi mbalimbali za Bazecha walieleza jinsi watakavyotumia nafasi hizo kuliheshimisha baraza hilo, iwapo wajumbe watawaridhia na kuwapa kura za kuwawezesha kushika nyadhifa walizoomba.

Shughuli ya kujinadi ilianza saa 10:45 jioni na kumalizika saa 12:15 jioni. Kila mgombea alipewa dakika moja ya kujieleza na kuulizwa maswali matatu, ambayo kila mgombea aliyajibu huku wajumbe wakisikiliza kwa makini.

Baadhi ya maswali yaliyoonekana kuwa magumu yalihusu mabadiliko ya Katiba, ambapo mwenyekiti wa muda wa mkutano huo alitoa muongozo kwamba suala hilo limeshajibiwa na viongozi wakuu wa chama.

Katika kujinadi, wagombea wameeleza changamoto walizopitia kwa utumishi wao ndani ya Chadema, zikiwemo kukosa ajira na mshahara. Wote wamesisitiza dhamira yao ya kuimarisha chama na kukisaidia kushika dola.

Baadhi ya wagombea wamesema nafasi walizoomba ni turufu yao ya mwisho kutumikia chama, wakizingatia umri wao mkubwa. Pia, imebainika hoja kwamba Bazecha haina nguvu ikilinganishwa na Bavicha, na baadhi ya wagombea wamependekeza mabadiliko ya kimuundo ili kulipa nguvu baraza hilo.

Hoja nyingine iliyozua mjadala ni madai kuwa wazee hawakopesheki kwa sababu ya umri wao. Hata hivyo, mgombea mmoja ameahidi kuongoza mapambano ya kudai haki za wazee, ikiwa ni pamoja na maandamano ya amani.

Wagombea walipoulizwa kuhusu matusi yanayolengwa kwa wazee kupitia mitandao ya kijamii, wameeleza kwamba watajikita kwenye maadili na kushirikiana na viongozi wengine kuhakikisha heshima inarudi.

Wagombea na nafasi wanazoomba

Nafasi ya mwenyekiti inagombewa na Hashim Juma Issa, anayepigania kutetea nafasi hiyo, huku akichuana na Suzan Lyimo, John Mwambigija, Hugo Kimaryo, na Mwerchard Tiba.

Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, mgombea pekee ni Shaban Madede. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar inawaniwa na Mohamed Ayoub Haji na Hamoud Said Mohamed.

Waliojitokeza kuwania Ukatibu Mkuu wa Bazecha ni Dk Leonard Mao, Hellen Kayanza, na Casmir Mabina, aliyewahi kuwa Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani.

Kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, wagombea ni Hamid Mfaligundi na Omary Mkama, huku nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar ikiwaniwa na mgombea pekee, Rajab Khamis Bakari. Nafasi ya Mweka Hazina imechukuliwa na mgombea pekee, Florence Kasilima.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi kuhusu uchaguzi huu.

Related Posts