Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa chama hicho (Bazecha) kumkataa “shetani” anayetaka kukifarakanisha chama hicho, huku akisema kukiangamiza chama hicho ni sawa na uhaini kwa kuwa kimebeba maono ya Watanzania wengi wanaokumbana na changamoto mbalimbali.
Mbowe amesema hayo leo Jumatatu, Januari 13, 2025, wakati wa hotuba yake kwenye mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Mbowe aliambatana na makamu wake-Bara, Tundu Lissu, katika mkutano huo. Mbowe na Lissu pia ni wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.
Miamba hiyo miwili kuwania nafasi moja ya juu imeibua mivutano mikali ndani na nje ya chama hicho. Hata hivyo, wote wawili wamekuwa wakisisitiza mshikamano na sasa wametoka na kaulimbiu ‘Stronger together’ ikiwa na maana “Imara pamoja.”
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo wa Bazecha unatarajia kuchagua viongozi wapya watakaoliongoza baraza hilo kwa miaka mitano ijayo.
Wanaowania nafasi ya uenyekiti wa Bazecha ni Hashim Juma Issa anayetetea nafasi hiyo, akichuana na wagombea wanne, akiwemo Suzan Lyimo, ambaye ni makamu wake-Bara.
Wengine kwenye nafasi hiyo ni John Mwambigija, Hugo Kimaryo na Mwerchard Tiba.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Bara, amejitokeza Shaban Madede pekee, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar ikiwania na Mohamed Ayoub Haji na Hamoud Said Mohamed.
Walioteuliwa kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Bazecha ni Dk Leonard Mao, Hellen Kayanza na Casmir Mabina, ambaye aliwahi kuwa Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani.
Kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, wanaowania ni Hamid Mfaligundi na Omary Mkama, wakati upande wa Zanzibar ni Rajab Khamis Bakari, mgombea pekee, sawa na Mweka Hazina, Florence Kasilima.
Mbowe amesema chama hicho kimepitia changamoto kubwa, akibainisha mnyukano unaoendelea kwa sasa katika kusaka nafasi za uongozi.
“Wote ni mashahidi, kwa miaka saba chama hiki kilijaribiwa kwa kila aina. Tulitupiwa mashetani ya kila aina, na haikuwa kwetu pekee bali hata kwa vyama vingine vya upinzani. Lakini kwetu tulibaki kuwa mashujaa.
“Majaribu yalikuwa mengi, kwa wabunge, madiwani, na hata kuna waliopoteza uhai kwa ajili ya kukipigania chama hiki. Nawataka wazee muendelee na ustahimilivu na kujivunia kwa kuwa mlisimama imara kukipigania. Wanaotaka kutufarakanisha na mashetani yao, tuwakatae, kwani itakuwa laana, na kukiua chama hiki itakuwa uhaini,” amesema Mbowe.
Ameongeza kuwa safari ya Bazecha haijawahi kuwa rahisi, kwani walikumbana na milima na mabonde, wakiumwa na ng’e lakini walivumilia na hatimaye kufika hapo.
“Na sasa tunaanza mserereko wa uchaguzi na safari ambayo itatupeleka hadi Januari 23 tutakapohitimisha. Tumekuwa tukishuhudia minyukano ya kila aina mitandaoni, lakini lazima tutambue kuwa chama hiki ni kikubwa kuliko mtu binafsi. Kimebeba ndoto za watu wengi wa Chadema na waliopo nje,” amesema Mbowe.
Amesema kukiangamiza chama hicho ni uhaini kwa kuwa chama hicho kimebeba maono ya Watanzania wanaopambana na changamoto mbalimbali.
“Wakati nakabidhiwa uongozi wa chama hiki miaka 21 iliyopita, hakukuwa na Baraza la Wazee, itifaki wala kanuni. Hivyo ni wajibu kwa kila mmoja anayeona ana maoni, milango iko wazi,” amesema.
“Chama hiki si cha Mbowe pekee. Chama hiki si Biblia. Nyaraka za chama hiki zinafanyiwa rejea na kubadilishwa. Tuache kutengeneza fitina,” amesema Mbowe.
Aidha, amewataka watu kuacha kuona uzee kama laana kwa kuwahukumu wazee kwa umri wao, badala yake watazamwe kama maktaba muhimu.
“Kuna vijana wa miaka 20 lakini akili zao zinafanana na wazee wa miaka 80. Tuwaeshimu wazee. Wazee walihudumu kukijenga chama hiki. Tusiwahukumu kwa kuonekana si chochote bali tuheshimu michango yao kwa kutufikisha hapa,” amesema.
Awali, katika mkutano huo, Tundu Lissu amesema:
“Naomba niwashukuru waliotumikia nafasi hii kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Lakini naamini leo tutapata safu mpya ya kujenga matofali. Wakati huu, baada ya leo nitakuwa na miaka 58. Wazee wenzangu, heri ya mwaka mpya kwa wale ambao hatujakutana.”
“Naomba nisiwapotezee muda. Niwatakie kila la heri. Tuchague viongozi kwa uchaguzi ulio huru na wazi kama inavyosema Katiba yetu ili waongoze kwa miaka mitano ijayo,” amesema Lissu.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama amewataka wajumbe hao kutumia demokrasia kwa tija kuchagua viongozi wenye maono.
“Tambueni mkifanya vibaya jahazi hili likijaa itachukua muda kurudisha uhai wake, demokrasia tunayozungumzia imeasisiwa na nchi za magharibi zinaruhusu kwa kuweka mifumo ya kuchaguana kupata viongozi wa kuwakilisha wengi, hivyo mtakaochukua kijiti tambueni mnayo majukumu mengi,” amesema.
Kabla ya Mbowe kuwasili kwenye mkutano huo, Lissu aliwasili saa 6:33 mchana na kuibua shangwe kutoka kwa wajumbe.
Kuingia kwa Lissu kulisababisha wajumbe wote kusimama na kushangilia huku wakiimba: “Lissu! Lissu! Lissu!” kisha wakaendelea: “Heche! Heche! Heche…!”
Shangwe ziliendelea hadi Lissu alipoketi katika kiti alichoandaliwa meza kuu ndipo wajumbe walipoketi katika nafasi zao.
‘Hatuuzi chama,’ ‘hatuhami chama,’ ‘tumejipata,’ na ‘Stronger Together’ ni salamu zilizotolewa na kanda mbalimbali kila wajumbe wake walipoinuliwa kwa ajili ya utambulisho.
Hadi saa 6:48 mchana, Mbowe alikuwa hajafika ukumbini hapo.
Kwa sasa Mbowe na Lissu wamekwenda katika mkutano mkuu wa Bavicha unaofanyikia ukumbi wa Ubungo Plaza.
Imeandikwa na Baraka Loshilaa, Tuzo Mapunda, Juma Issihaka na Bakari Kiango
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.