Wananchi Mbinga waomba zahanati yao ifunguliwe haraka

Mbinga. Wananchi wa Kijiji cha Mundeki, Kata ya Muyangayanga, Wilaya ya Mbinga, wameiomba Serikali kuharakisha kupeleka wataalamu wa afya na vifaa tiba katika zahanati yao ili huduma za afya zianze kutolewa.

Wananchi hao wamesema ukosefu wa huduma hiyo umewalazimu kusafiri umbali mrefu, jambo linalosababisha changamoto kubwa, hasa kwa wagonjwa na wanawake wajawazito.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 13, 2025, katika eneo la zahanati hiyo, wamesema jengo hilo limekamilika lakini linaendelea kusubiri wataalamu na vifaa tiba.

Marietha Kinunda, mkazi wa Kijiji cha Mundeki na mhudumu ngazi ya jamii kutoka Zahanati ya Kindimba, amesema zahanati hiyo ilijengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali, ambapo Serikali imesaidia baadhi ya vifaa vya ujenzi.

Hata hivyo, amesema kilichobaki sasa ni ujenzi wa vyoo, ambao uko katika hatua za mwisho.

“Zahanati hii imejengwa kwa juhudi kubwa. Tumeshuhudia vifo vya watu waliotarajia kupata huduma hapa, lakini walikosa. Tunaomba kabla ya Februari mwaka huu huduma za matibabu zianze kutolewa hapa,” amesema Kinunda.

Petrol Hyela, Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho, ameipongeza Serikali kwa hatua za ukamilishaji wa zahanati hiyo lakini akaomba ifunguliwe haraka ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wanawake wajawazito ambao wanajifungulia njiani, hali inayozidi kuwa mbaya wakati wa mvua.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa sasa wa Kijiji cha Mundeki, Pius Ndunguru, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wataalamu wa afya wanapelekwa haraka kijijini hapo ili zahanati ifunguliwe.

Amebainisha kuwa wananchi wanalazimika kufuata huduma za afya katika zahanati ya Kindimba iliyopo umbali wa kilomita nane au katika Kijiji cha Litembo, kilomita 12 kutoka Mundeki.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mbinga, Sheila Mbike, amesema Halmashauri ya Mji wa Mbinga inaendelea kuboresha miundombinu ya afya ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora.

Amesema zahanati hiyo itakapofunguliwa, itatoa huduma za uhakika kwa wakazi wa Mundeki, ambao ni takribani watu 1,500.

“Zahanati ya Mundeki itaimarisha huduma za afya, hasa kwa mama na mtoto, na kuwawezesha wananchi kupata matibabu kwa urahisi. Vifaa tiba tayari vipo kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 na zimeshapokelewa. Tuna hakika Februari, 2025 huduma zitaanza kutolewa,” amesema Mbike.

Wananchi wameeleza matumaini makubwa kwamba hatua za haraka zitachukuliwa ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa huduma za afya kijijini humo.

Related Posts