Musoma. Washiriki wa kozi ndefu kutoka Chuo cha Taifa Cha Ulinzi (NDC) wamefika mkoani Mara kwa ajili ya ziara ya siku tano ya mafunzo kwa vitendo kuhusu masuala ya kiusalama ambapo pamoja na mambo mengine wanatarajia kufanya uchambuzi juu ya uwiano wa utekelezaji wa sera ya maendeleo katika maeneo yanayohusisha usalama wa taifa.
Mkuu wa Chuo hicho, Meja jenarali Augustine Ibuge amesema mjini Musoma leo Jumatatu Januari 13,2025 kuwa ziara hiyo ya siku tano inayohusisha washiriki 15 wa kozi hiyo wakiwepo 10 ambao ni maofisa waandamizi wa jeshi la wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama, idara na taasisi mbalimbali nchini huku wengine watano wakitoka nchi marafiki
Amesema katika ziara hiyo wanatarajia kuangalia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kukuza uchumi wa nchi na wananchi na namna ambavyo shughuli hizo zinachangia katika kuimarisha usalama wa nchi na watu wake.
“Tunataka kuangalia kama kuna viwanda na vinafanyaje kazi,kuna masuala ya kilimo,uvuvi bila kusahau masuala ya utamaduni vyote hivyo tunataka kuona vinatuunganishaje kama mkoa na watanzania kwa ujumla katika kuimarisha usalama wa nchi yetu,” amesema
Amesema suala la usalama wa nchi sio jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama pekee bali linawahusu wananchi wote katika nafasi zao ambapo amesema utekelezaji mzuri wa sera za maendeleo ni moja ya nyenzo inayoweza kutumika vema katika kuimarisha ulinzi wa nchi.
Amesema katika baada ya ziara hiyo watatoa maoni na mapendekezo juu ya ufumbuzi wa changamoto watakazozibaini ili kuwapa fursa wasimamizi wa sera kuboresha utendaji wao wa kazi lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wananufaika na sera za maendeleo ambazo zitakuwa na mchango chanya kwenye suala zima la ulinzi na usalama wa nchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Meja Jenerali Ibuge amewataka watumishi wa hospitali hiyo kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji kwa maelezo kuwa huduma bora za afya ni moja ya kichocheo cha ulinzi na usalama wa nchi.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa hospitali hii pamoja na ununuzi wa vifaa tiba kwahiyo wananchi wanatarajia kupata huduma bora na niwaambie tu kuwa upatikanaji wa huduma bora una mchango mkubwa sana katika kuimarisha usalama wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amewataka washiriki hao kuwa mabalozi wa mkoa huo kwa kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji zilizopo mkoani humo.
Amesema serikali imejitajidi kuwekeza na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii mkoani humo na kwamba ujio wa washiriki hao kwa namna moja ama nyingine utakuwa chachu ya kuboresha huduma zinazotolewa katika idara na taasisi za serikali.
“Tunatarajia kupata maoni yenu juu huduma zetu, kwani maoni hayo yatasaidia kutuonyesha wapi tunafanya vizuri na wapi tunatakiwa kuongeza jitihada kwani huduma bora za kijamii zina mchango mkubwa katika ulinzi na usalama wa nchi,” amesema Mtambi
Mmoja wa washiriki hao, Nikodemas Kapinga amesema wakati wa ziara hiyo watapata fursa ya kuangalia utekelezaji wa masuala ya sera kwa vitendo baada ya kusoma kwa nadharia ambapo wanatarajia kupata fursa pia ya kujadiliana na wasimamizi juu ya namna ya kuboresha pale ambapo watabaini pana mapungufu.
“Tunaangalia kama yale yaliyoandikwa kwenye makaratasi yanatekelezwa kwa vitendo kwani tayari tumesoma sera mbalimbali ambazo zina mchango mkubwa katika ulinzi na usalama wa nchi lakini sera hizo kama hazitekelezwi kwa vitendo basi itakuwa ni kazi bure,” amesema