Waziri Ulega atoa maagizo ERB

Morogoro. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) nchini kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali za kiuhandisi, hasa katika miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wa kazi zao.

Akifungua baraza la wafanyakazi wa bodi hiyo, lililokutana mkoani Morogoro kujadili masuala mbalimbali, Ulega ameeleza kuwa wahandisi ni moja ya kada muhimu katika maendeleo ya Taifa, na ni muhimu kuwa na mfumo maalumu utakaowezesha ufuatiliaji wa utendaji kazi wao.

“Natoa maelekezo matatu yatakayowezesha tasnia hii kufikia malengo mliyoyaweka. Kwanza, bodi iongeze juhudi katika kushirikisha Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu, na mashirika ya kimataifa. Pili, wekeni mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na maendeleo yake kwa wakati. Tatu, hakikisheni wahandisi wachanga wanashiriki kikamilifu katika miradi yenu,” amesema Waziri Ulega.

Aidha, Waziri Ulega ameiagiza Bodi ya Wahandisi kuimarisha programu za kuwaendeleza vijana katika tasnia hiyo, ili kuhakikisha wanazalisha wahandisi wenye uwezo wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la kitaifa na kimataifa.

“Ni lazima wahandisi wabadilike kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, hasa mkiwekeza nguvu kwa vijana, kuongeza ubunifu katika kazi zenu, na muhakikishe mnailinda heshima ya fani ya uhandisi ili iendelee kuwa na taswira nzuri katika jamii,” amesema Waziri Ulega.

Awali, akitoa taarifa kuhusu hali ya Bodi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, ambaye pia ni Msajili wa Wahandisi, Mhandisi Bernard Kavishe, amesema bodi hiyo inasimamia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kusajili wahandisi wenye maadili na weledi katika utendaji kazi wao.

Mhandisi Kavishe ameeleza kuwa bodi inasimamia miradi mbalimbali, ikiwemo mradi wa uwezeshaji wa shule ya uhandisi yenye programu ya kuchagiza sayansi na hisabati kwa vijana, ikizingatia jinsia. Aidha, amefafanua kuhusu mpango wa atamizi kwa vijana unaotoa elimu ya ujasiriamali, ambapo unatarajiwa kunufaisha vijana zaidi ya 100 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Related Posts