Wenyeviti wa mitaa Arumeru kusaka watoto wasiopelekwa shule

Arusha. Viongozi wa Serikali za mitaa, wakiwemo wenyeviti katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, wamepewa jukumu la kufanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini na kutoa taarifa za watoto wote wenye umri wa kwenda shule ambao hawajapelekwa.

Serikali imetoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 13, 2025, siku ya kufunguliwa shule zote nchini, huku wazazi na walezi wenye watoto waliotimiza umri wa kwenda shule wakiendelea kuwaandikisha.

Akizungumza na wenyeviti na watendaji, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amri Mkalipa, amesema hatarajii kupata malalamiko kuhusu watoto waliotimiza umri wa kuanza shule na hawakupelekwa, wakati kazi ya uandikishaji itakapokamilika.

“Hivi karibuni nitaanza ziara ya kijiji kwa kijiji, mtaa kwa mtaa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wangu. Sasa nisifike huko nianze kusikia moja ya kero ni kwamba kuna watoto waliofika umri wa kwenda shule na hawakupelekwa. Kiukweli, viongozi wa mtaa huo hatutaelewana,” amesema Mkalipa na kuongeza:

“Nendeni mkaanze kibarua hicho mapema kuhakikisha kila nyumba ya mwananchi wenu watoto wanaenda shule, bila kuletwa kwa kisingizio chochote eti amekataliwa kwa sababu hana madaftari au sare za shule.”

Mkalipa amesema kwa Wilaya ya Arumeru, Serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha miundombinu ya elimu ili kufuta ujinga miongoni mwa wanafunzi.

“Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) amewekeza fedha nyingi katika miundombinu yetu kwa ajili ya kusaidia watoto wetu wapate elimu. Zungumzeni na wananchi wenu huko, maana wazazi nao lazima wajibu kisheria kwanini hawajapeleka watoto wao shule wakati umri wa kusoma anao.”

Mkalipa amesema yuko tayari kugharamia baadhi ya madaftari na sare za shule kwa wanafunzi wasio na uwezo wa kununua ili kuhakikisha wote wanapata nafasi ya kusoma.

“Kwenye maandiko imeandikwa Mungu ni mume wa wajane na yatima. Sasa msifikiri huyo Mungu atashusha mahitaji ya hawa watu. Mimi nimeguswa na Mungu, niko tayari anitumie kuwahudumia wasiojiweza.

“Na wewe ukiguswa huko kwako, fanya tendo hilo kama sadaka ya mwaka mpya. Lakini wale mtakaoshindwa kabisa, waleteni ofisini kwangu, mimi nitawasaidia,” amesema Mkalipa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Majimoto, Mariaki Mollel, amesema wamepokea maelekezo ya mkuu wa wilaya na wako tayari kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanawasilishwa.

“Hilo suala tulishalianza kwa kuwahamasisha wazazi wenye watoto wakawaandikishe tangu wiki iliyopita. Hivyo kwa sasa tunakwenda tena kupita nyumba kwa nyumba kwa kushirikiana na mabalozi wetu kuona kama kuna waliobaki, na changamoto ni nini ili itatuliwe mapema wasipitwe na masomo,” amesema mwenyekiti huyo.

Related Posts