BAADA ya kukaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti, hatimaye kiungo mshambuliaji wa Fountain Gate Princess, Winifrida Charles, amerejea akicheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Boni Consilli Girls ya Uganda.
Kiungo huyo alipata majeraha ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja kwa takribani msimu mmoja na nusu.
Winifrida alionyesha kiwango bora kwenye mashindano ya GIFT akiwa na TDS Academy akiazimwa kutokea Fountain na mchezo wa kwanza alifunga kwenye ushindi wa mabao 2-0.
Akizungumzia juu ya urejeo wake, kinda huyo alisema anatamani kurejea kwenye ubora wake haraka kuisaidia timu yake baada ya kukaa nje muda mrefu.
“Unapokuwa nje ya uwanja muda mrefu unaporudi hauwi sawa kama mwanzo, natamani nirejee haraka, hakuna kitu kigumu kama mchezaji kupitia majeraha,” alisema Winifrida.
“Kwenye haya mashindano natamani niwe mfungaji bora, tunapambana ili tuweze kuonekana.”