MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2025 inafikia tamati usiku wa leo wakati timu za taifa za Zanzibar Heroes, wenyeji wa michuano hiyo, na wageni Burkina Faso zitapovaana katika fainali ya kisasi kwenye Uwanja wa Gombani, visiwani Pemba.
Zanzibar na Burkina Faso zinakutana tena kuanzia saa 1:00 usiku baada ya awali kuvaana katika mechi ya makundi na wageni kushinda kwa bao 1-0, hivyo leo ni zamu ya wenyeji kujitutuma na kulipa kisasi ili kuzuia taji la michuano hiyo lisiondoke nchini au iteleze tena na kuwa jamvi la wageni ikikosa kila kitu licha ya uenyeji wao.
Bingwa wa michuano hiyo iliyoanza tangu Januari 3 ikishirikisha timu za taifa badala ya klabu kama ilivyozoeleka atabeba ubingwa sambamba na zawadi ya Sh100 milioni, huku wageni wakionekana kuwa na nafasi nzuri kutokana na rekodi tamu waliyoiweka hadi sasa ikiwa ndio timu pekee isiyoonja kipigo.
Timu nne za mataifa ya Kenya, Burkina Faso, Tanzania Bara na Zanzibar ndio zilizoshiriki hatua ya awali baada ya nchi za Uganda na Burundi kujitoa katika dakika za mwishoni, ambapo Burkina Faso ilimaliza kinara wa msimamo ikivuna pointi saba, mabao manne ya kufunga na kufungwa moja katika mechi tatu.
Wenyeji Zanzibar walimaliza wa pili katika msimamo wakiwa na pointi sita kupitia mechi tatu pia, wakishinda michezo miwili na kupoteza moja, wakifunga mabao mawili na fungwa moja, mbele ya Kenya iliyomaliza ya tatu kwa alama nne, huku Kilimanjaro Stars ya Bara ikiburuza mkia bila pointi wala bao lolote.
Katika mchezo huo Zanzibar itaendelea kumtegemea nahodha, Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye bao moja na asisti moja vilevile katika kuhakikisha inalibakiza taji hilo visiwani Zanzibar ili kunogesha sherehe za Siku ya Mapinduzi iliyoadhimishwa jana Jumapili ikiwa ni miaka 61 tangu yalipofanyika Januari 12, 1964.
Mbali na Fei Toto, timu hiyo ya Zanzibar itakayomkosa beki wa kati Ibrahim Ame aliyelimwa kadi nyekundu katika mechi iliyopita dhidi ya Kenya, itawategemea pia Ibrahim Hamad ‘Hilika’, Maabad Maulid, Khatib Idd ‘Gego’ na wengine kuwabana Burkina Faso wanaomtegemea zaidi Clement Pitroipa.
Nyota huyo wa Burkina Faso ndiye kinara wa mabao kwa sasa wa michuano hiyo akifunga mawili alipoizamisha Kilimanjaro Stars kwa mabao 2-0, lakini ina mastaa wengine wenye vipaji ambao wanafaa kuchungwa kama wenyeji wanataka kulibakiza kombe na fedha hizo za Mapinduzi 2025.
Haitakuwa mechi rahisi kwa timu zote kutokana na aina ya soka lililochezwa kwenye mechi za hatua ya awali, lakini Zanzibar Heroes ikiwa na kazi kubwa ya kuwazuia Waburkinabe ambao wanacheza soka la kasi na la nguvu, ili kuweka heshima mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi wa fainali hiyo inayohitimisha siku 11 za michuano hiyo ya Mapinduzi 2025.
Msimu uliopita, Mlandege ilitetea ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya kuifunga Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya fainali, baada ya mwaka 2023 kuinyoa Singida Big Star kwa mabao 2-1.