Beki Dodoma Jiji aingia chimbo kujifua

BEKI wa Dodoma Jiji FC, Anderson Solomon ameweka wazi anajipanga vyema kuhakisha anapambania namba katika kikosi hicho pindi Ligi Kuu Bara itakapoendelea Machi Mosi mwaka huu.

Nyota huyo ambaye amekuwa na kikosi hicho tangu msimu uliopita, mambo yamekuwa magumu kwake baada ya kukutana na upinzani mzito kutoka kwa Dickson Mhilu katika nafasi anayocheza ya beki wa kulia.

Kutokana na ushindani aliokumbana nao, ametumika kwa dakika 30 pekee akicheza mechi mbili na zote akitokea benchi kati ya mechi 16 za ligi ambazo timu hiyo imecheza msimu huu.

Mechi hizo ni dhidi ya Singida Black Stars ambayo Dodoma Jiji FC ilipoteza kwa mabao 2-1 na dhidi ya Yanga SC ambayo walipoteza tena kwa mabao 4-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Solomon alisema mikakati yake kwa sasa ni kupata nafasi ya kucheza kwa muda mrefu kama ilivyokuwa msimu wa 2023-2024 ambao alikuwa na kiwango bora.

“Mwaka uliopita siwezi kusema kama ulikuwa mgumu kwangu maana sikupata tu nafasi ya kucheza ila mwaka huu nimeamua kujifua ili ligi ikiendelea nipate namba,” alisema Solomon.

Akizungumzia mechi 16 ambazo Dodoma Jiji FC imecheza hadi sasa na namna ushindani ulivyo, alisema ligi ni ngumu kwani kila timu imesajili vizuri huku akibainisha bado wana nafasi kubwa ya kumaliza katika nafasi tano za juu na kutimiza malengo waliyojiwekea.

Dodoma Jiji FC inashika nafasi ya tisa kwemye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 19 baada ya kucheza mechi 16, imeshinda tano, sare nne na kupoteza saba huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu 21.

Related Posts