Bibi adaiwa kujiua kwa kunywa sumu Rombo

Moshi. Mkazi wa Kijiji cha Kibaoni, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Theodora Nisetas anayekadiriwa kuwa na miaka 65, anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu huku chanzo kikiwa bado hakijajulikana.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuzungumzia tukio hilo, aliomba apewe muda kulifuatilia kama limeripotiwa polisi wilayani humo.

Inadaiwa kuwa, jaribio la Theodora kutaka kujiua si mara ya kwanza kulifanya, na la pili alilifanya jioni Januari 12, mwaka huu na alifariki duniani alfajiri ya Januari 13, 2025 wakati akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha Karume.

Inadaiwa kuwa, bibi huyo anayeishi na msichana wa kazi, alimtuma msichana huyo dukani kumnunulia vocha na aliporejea alikuta matapishi sebuleni na pembeni yake kukiwa na mfuko unaodhaniwa kuwa na sumu.

Inadaiwa kuwa, msichana huyo alipomtafuta alimkuta bibi huyo kajilaza kwenye miti uliopo nyumbani hapo, huku akiwa na hali mbaya.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Herment Kimario amesema tukio hilo lilitokea Januari 12, 2025.

Amesema miaka ya nyuma bibi huyo aliwahi kufanya jaribio la kutaka kujiua na aliokolewa.

“Ni kweli tukio hili limetokea hapa kijijini kwangu, huyu mama alikunywa sumu Jumapili na taarifa nilizonazo, amefariki alfajiri ya jana Januari 13, wakati akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha Karume,”amesema.

 “Huyu mama sio mtu mwenye changamoto au mtu ambaye amekosa chochote, ni mama anayejituma kwenye kazi na ana watoto wenye uwezo na kwenye jamii sijaona kama ana ugomvi wowote na mtu.”

Mmoja wa wanakijiji, Damian Tesha amesema tukio hilo limewaumiza kwa kuwa bibi huyo alikuwa hana changamoto yoyote ya kimaisha.

“Kwa kweli kifo cha huyu mama kimetuumiza sana, ni mtu anayeishi maisha mazuri hana shida yoyote, lakini hatujui ni kitu gani kimemkumba kwa kweli, ni mtu ambaye ana rasilimali za kutosha,”amesema.

Mwili wa bibi huyo umehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Karume wilayani humo.

Related Posts